Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchezaji ligi kuu Tanzania awekwa karantini

102241 Pic+karantini Mchezaji ligi kuu Tanzania awekwa karantini

Mon, 13 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiungo wa timu ya soka ya KMC ya jijini Dar es Salaam, Jean Mugiraneza amewekwa karantini baada ya kurejea kutoka nchini kwao, Rwanda.

Katika kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, Serikali imeweka utaratibu wa kuwaweka karantini kwa gharama zao watu wote wanaoingia kutoka mataifa ya nje bila kujali kama ni raia au sio raia.

Mwananchi limethibitishiwa kwamba mchezaji huyo amekutana na karantini baada ya kutua nchini Aprili Mosi akitokea kwao kwa kutumia usafiri wa gari.

Ofisa mtendaji mkuu wa KMC inayoshiriki Ligi Kuu Bara, Walter Harrison jana alikiri kuwa mchezaji huyo yupo karantini kwenye hosteli za Magufuli zilizopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kweli Migi yupo karantini katika hosteli anaangaliwa, si unajua ametoka nje, lakini yupo sawa ila anafuata utaratibu uliowekwa,” alisema Harrison.

Akizungumzia wachezaji wengine wa ndani alisema kila mchezaji anaendelea na mazoezi nyumbani kwake.

Pia Soma

Advertisement
“Hawa wa ndani wapo kwenye tahadhari ambayo kila mmoja anayo, wapo kwao wanaendelea kujilinda na wa nje wapo kwao.” Baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu waliosafiri kwenda kwao nje ya nchi ni Francis Kahata aliyekwenda Kenya, Meddie Kagere (Rwanda), Clatous Chama (Zambia), Luis Miquissone (Msumbiji) - wote wanaoichezea Simba. Kwa upande wa Yanga ni Lamine Moro (Ghana), ilhali Azam ni Razack Abalora, Yakub Mohammed, Daniel Amoah (wote wapo Ghana) na huenda wote watakaporejea wakafikia karantini.

KARIA ALIONYA

Mapema baada ya ligi kusimamishwa, rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliziambia klabu kuwa endapo zitawaruhusu wachezaji wao wa kigeni kurejea katika nchi zao, hawatawaruhusu tena kurejea na kushiriki Ligi Kuu moja kwa moja.

Karia alisema TFF haijatoa likizo kwa wachezaji, bali Serikali imesimamisha michezo kwa lengo la kupambana na janga la corona, hivyo klabu zisitumie mapumziko ya siku 30 za ligi kama likizo.

“Tunazikumbusha klabu na viongozi wake kuwa hatukutoa likizo kwani nimeshapata taarifa kuna baadhi ya klabu zina wachezaji wa kigeni au wafanyakazi wanafanya matayarisho ya kuwaruhusu kwenda kwenye nchi zao, sasa hiyo itakuwa ni kinyume na maelekezo ya Serikali,” alisema.

“Si ajabu tayari kutakuwa na hali ya unafuu lakini wao wametoka huko hatujui wametoka wapi, ila hatuwaruhusu kushiriki kwenye michezo yetu na tutawasiliana na vyombo vya Serikali kuhakikisha hatuwaruhusu kurudi tena nchini kwa kipindi hiki ambacho tutakuwa kwenye tahadhari.

“Ni mwezi wa kuhakikisha maambukizi yasiendelee na hali ikiwa nzuri tunaweza kuendelea na shughuli zetu za kawaida, sasa tukiendelea halafu tulishawaruhusu watu wakaenda kwenye nchi zao na hatujui tahadhari ambazo nchi hizo zilichukua, zimeathirika vipi, hivyo tukithubutu kuwaruhusu tu tutakuwa kama tunafanya mchezo.”

Aliyekuwa ofisa habari wa Uhamiaji, Ally Mtanda alisema wameongeza muda wa vibali vya wachezaji na makocha wa kigeni kutokana na janga la corona duniani.

“Sio wao tu, bali wageni wote walioingia hapa nchini ambao muda wao wa kukaa umeisha na hawawezi kurejea kwao.”

Chanzo: mwananchi.co.tz