Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Mexico (FMF) limeanzisha uchunguzi baada ya kusambaa kwa kipande cha video kikimuonesha mwamuzi akitumia goti lake kumpiga sehemu za siri mchezaji wakati wa mechi ya Club America dhidi ya Leon siku ya Jumamosi.
Kipande cha video kinamuonesha mwamuzi, Fernando Hernandez akimpiga na goti Kiungo wa Leon, Lucas Romero wakati mchezaji huyo na wenzake walipokuwa wakitaka VAR irudie upya tukio la goli la kusawazisha lililofungwa na Club America.
Tume ya Waamuzi imesema matokeo ya uchunguzi huo yatawekwa hadharani utakapokamilika.
Iwapo Hernandez atapatikana na hatia inasemekana anaweza kukabiliwa na faini na kufungiwa kati ya mechi moja hadi 15 chini ya sheria za Liga MX.
Licha ya vyombo vya habari nchini Mexico kulaani kitendo hicho mchezaji mwenyewe, Lucas Romero ametaka mwamuzi huyo asipewe adhabu na kusema tukio hilo halikuwa la kukusudia.