Wakati Simba wakikubali kichapo cha goli 1-0 Juzi Jumamaosi kutoka kwa Wydad mchezo wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wengi wameonekana kuipongeza Simba kutokana na soka safi walilocheza chini ya Kocha mpya Benchikha.
Sasa Mtangazaji na mchambuzi wa michezo kutoka Clouds FM, David Kampista yeye ameonekana kuja na mawazo tofauti kutoka na kipigo hicho cha Simba ugenini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Kampista ameandika;
"TUNAIPAKA SIMBA MAFUTA tena kwa mgongo wa chupa, binafsi siwezi kuisifia Simba kwa mechi ya juzi utakuwa ni unafiki uliopitiliza"
"Kwa mtazamo wangu Simba wamejaribu kujitutumua kutokana na hali waliyonayo, bado ujio wa Kocha mpya umewashtua tu wachezaji ambao wanaiwazia hatma yao baada ya msimu kumalizika kwa kuwa lazima mikataba ya baadhi yao inakaribia kumalizika, wanapambana tu lakini ukweli ni kwamba kiwango chao kwa sasa hakiwezi kuivusha Simba katika daraja refu la kucheza nusu fainali ya Klabu bingwa Afrika."
"Naona watu wanaimwagia sifa Simba kwa mechi ya juzi, ghafla wamesahau Simba walijitutumua dhidi ya Wydad ambaye ana shida zake laki tisa milioni na bado mnyama akafa katika mechi yenye hesabu kali kupita mfano."
"Kwa kifupi tangu msimu uliopita Simba alifuzu robo fainali kwa tabu mno! lakini bado wenye timu ni kama hawakujifunza kwa aina ya sajili wanazozifanya, mwisho wa siku mzigo wa lawama huwa unabakia kwa makocha!"
"Simba kwa sasa sajilini katika Klabu zinazocheza makundi katika michuano hii mara kwa mara na sio kuokoteza au kununua maveterani mnajiumiza wenyewe! mpeni Benchikha madirisha kadhaa awatengenezee timu, mkichelewa anguko lenu halipo mbali!"