Mchambuzi maarufu wa soka nchini kupitia channel ya runinga ya TV3, Alex Ngereza amesema kuwa baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa ligi dhidi ya KMC, kiungo mpya wa Yanga Sc, Pacôme Zouzoua anaweza kuwa mchezaji bora wa msimu wa Ligi ya NBC (MVP).
Zouzoua ambaye amesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea ASEC Mimosas ya nchini Ivory Coast ameonyesha kiwango bora katika mechi alizocheza hasa dhidi ya KMC huku akiisaidia timu yake kushinda bao 5-0 na yeye akiweka msumari wa mwisho.
"Pacome ni mchezaji mzuri sana binafsi niliposikia tetesi kuwa Yanga wanataka kumsajili sikuamini kama atakuja kucheza kwenye ligi yetu,akiendelea na kiwango hiki anachokionyesha basi anaweza kuwa MVP mpya wa msimu huu," amesema Mgereza.
Yanga sasa inahesabu alama tatu na bao 5 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu baada ya kucheza mchezo mmoja tu ambao unaonyesha Yanga wamedhamiria kutetea taji lao kama ambavyo wamekuwa wakijinasibu.
Aidha, Yanga leo itashuka Dimbani kusaka tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS FC ya nchini Djibouti huku Yanga ikiwa na faida ya bao 2-0 ilizofunga kwenye mchezo wao wa kwanza.