Mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Simba unepiga hatua baada ya kusimama kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa kamati ya Katiba na Sheria wa Simba, Hussein Kitta amesema wameshayafanyia kazi mambo sita ambayo yana faida kwa wanachama.
"Waziri mwenye dhamana ya michezo aliitisha kikao kujadili kuhusu mchakato wa mabadiliko wa Simba na kukawa na mambo sita ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.”
“Kutokana na mkutano huo [na waziri] bodi ya Simba ikaunda kamati hii. Tulipokea maoni mengi, mengine kwa barua pepe, mengine kwa barua, wengine kutupigia simu na kutumia ujumbe. Tulikaa vikao vinne kwa kati ya masaa 4-9.”
“Lengo ni kukamilisha mabadiliko na serikali ilitupa muda ili kukamilisha jambo hili. BMT walisema kabla ya kupeleka kwa wanachama mlete hiyo rasimu tupitie kwanza. Baada ya vikao tukaenda BMT na nina furaha kuwambia kwamba tumepokea barua kutoka kwao ya kuridhishwa na yale tuliyopitisha.”
“Mambo sita yaliyopitishwa yana faida zaidi kwa mwanachama wa Simba kuliko kwa mtu mwingine yoyote,” alisema Kitta.