Msimu wa Ligi Kuu Bara 2023-2024 umetamatika juzi Jumanne huku Kipa wa Coastal Union, Ley Matampi akiibuka kinara wa clean sheets akimpiga bao Djigui Diarra wa Yanga.
Matampi raia wa DR Congo, huu ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara na amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kitu ambacho kwake kinampandisha thamani.
Kipa huyo amemaliza akiwa na clean sheets 15 na kuwa mbabe wa kulinda vizuri nyavu za timu yake zisitikiswe na wapinzani, wakati Diarra akiwa nazo 14.
Matampi amechukua kijiti hicho kutoka kwa Diarra ambaye huu ni msimu wake wa tatu na tayari amekuwa kinara wa clean sheets kwa misimu miwili mfululizo. Kabla ya hapo, ulikuwa utawala wa Aishi Manula wa Simba, ambaye alifanya balaa tangu akiwa Azam misimu miwili ya mwisho kabla ya kuendeleza alipojiunga na Simba 2017.
Huu ukiwa ni msimu wa kwanza kwa Matampi tangu ajiunge na Coastal Union akitokea Klabu ya Jeunesse Sportive Groupe Bazan ya Congo, amekuwa kinara wa clean sheets baada ya kucheza mechi 24 kati ya 30 za ligi, sawa na dakika 2160 huku akifanya sevu 37.
Coastal Union pia imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kurudi kimataifa baada ya kupita takribani miaka 36.
Coastal imepata nafasi hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo na kufuzu ushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1989 iliposhiriki Kombe la Washindi Afrika na kuishia raundi ya kwanza. Baada ya hapo ndipo michuano hiyo ilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2004 ambayo Coastal inakwenda kushiriki.
Matampi mechi nne za kwanza za msimu hakucheza, lakini alipoanza safari ya kuzisaka clean sheets, alikutana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam mfungaji akiwa Feisal Salum na kipa huyo alishindwa kuokoa hatari akajikuta anawapasia Azam na kuruhusu bao hilo.
Wakati alipokosekana, golini alisimama Chuma Ramadhani, mwanzoni alidaka Justin Ndikumana kabla ya kutimkia Mtibwa Sugar.
Katika mechi zilizofuatia akafanya vizuri ikiwemo sevu za hatari dhidi ya Yanga na Simba, licha ya kupoteza mechi hizo lakini alifanya kazi kubwa sana ya kulinda lango lake.
Kwa upande Diarra ambaye amekamata nafasi ya pili kwa makipa waliokuwa na clean sheets nyingi msimu huu akiwa nazo 14, amecheza mechi 21 kati ya 30 sawa na dakika 1846 akiwa na sevu 19.
Diarra kuna wakati alikosekana uwanjani kuichezea Yanga kwa sababu tofauti ikiwemo kutumikia adhabu au kuchelewa kujiunga na wenzake kutokana na majukumu ya timu ya taifa akiwa kipa namba moja wa Mali.
Raia huyo wa Mali, amekuwa chachu kubwa ya Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya tatu mfululizo huku yeye akiwa golini kwani alijiunga na timu hiyo msimu wa 2021-2022 akitokea Stade Malien ya Mali. Huu ni msimu wake wa tatu.
Ndani ya Yanga, anapokosekana Diarra, anadaka Aboutwalib Mshery na Metacha Mnata.
Matampi mbali ya kuwa kinara wa clean sheets, pia ana rekodi bora zaidi ya kulinda lango lake kwa wastani wa mabao kwa mechi ukilinganisha na Diarra ingawa siyo kwa tofauti kubwa.
Katika mechi 24 za Matampi akiwa langoni ndani ya Coastal Union, kipa huyo Mcongomani ameruhusu mabao 11 sawa na asilimia 45.83, wakati Diarra pale Yanga ameruhusu mabao 10 katika mechi 21 alizocheza sawa na wastani wa asilimia 47.61.
Kitendo cha Matampi kuwa kinara wa clean sheets kinaashiria wazi makipa wazawa wameendelea kupigwa bao na wageni kwani huu ni msimu wa tatu mfululizo wageni wanaibuka kidedea.
MAKIPA WALIOMALIZA NA CLEAN SHEETS NYINGI LIGI KUU BARA 2023-24
15 - Ley Matampi (Coastal Union)
14 - Djigui Diarra (Yanga)
10 - Jonathan Nahimana (Namungo)
10 - Costantine Deusdedith (Geita Gold)
10 - Ayoub Lakred (Simba)
TAKWIMU ZA MATAMPI vs DIARRA LIGI KUU BARA 2023-24
Matampi Diarra
15 Clean sheets 14
24 Mechi 21
2160 Dakika 1846
37 Sevu 19
MECHI ZA MATAMPI LIGI KUU BARA 2023-24
1. Coastal 0 - 1 Azam
2. Ihefu 0 - 0 Coastal
3. Coastal 2 - 0 Mashujaa
4. Coastal 0 - 0 Namungo
5. Coastal 0 - 1 Yanga
6. Prisons 0 - 1 Coastal
7. Singida FG 2 - 1 Coastal
8. Coastal 3 - 1 Geita
9. Coastal 1 - 0 Kagera
10. JKT TZ 0 - 1 Coastal
11. KMC 0 - 0 Coastal
12. Coastal 1 - 0 Dodoma Jiji
13. Coastal 1 - 0 Mtibwa
14. Tabora 1 - 0 Coastal
15. Azam 1 - 1 Coastal
16. Coastal 1 - 2 Simba
17. Coastal 1 - 0 Ihefu
18. Yanga 1 - 0 Coastal
19. Coastal 0 - 0 Prisons
20. Coastal 2 - 0 Singida
21. Geita 0 - 0 Coastal
22. Kagera 1 - 2 Coastal
23. Coastal 0 - 0 JKT TZ
24. Coastal 0 - 0 KMC
MECHI ZA DIARRA LIGI KUU BARA 2023-24
1. Yanga 5 - 0 JKT Tanzania
2. Yanga 1 - 0 Namungo
3. Ihefu 2 - 1 Yanga
4. Geita Gold 0 - 3 Yanga
5. Yanga 3 - 2 Azam FC
6. Yanga 2 - 0 Singida FG
7. Simba 1 - 5 Yanga
8. Yanga 4 - 1 Mtibwa Sugar
9. Tabora United 0 - 1 Yanga
10. KMC 0 - 3 Yanga
11. Yanga 5-0 Ihefu
12. Yanga 1-0 Geita Gold
13. Azam FC 2-1 Yanga
14. Singida FG 0-3 Yanga
15. Yanga 2-1 Simba
16. JKT Tanzania 0-0 Yanga
17. Yanga 1-0 Coastal Union
18. Mashujaa 0-1 Yanga
19. Yanga 1-0 Kagera
20. Mtibwa 1-3 Yanga
21. Yanga 3-0 Tabora United