Baada ya Kagera Sugar kuinasa saini ya aliyekuwa straika wa Ihefu, Moubarack Amza kwa mkataba wa miaka miwili, nyota huyo amesema kazi iliyobaki ni kuonyesha kiwango bora kikosini kufuatia kuanza vibaya msimu huu.
Nyota huyo raia wa Cameroon amejiunga na timu hiyo baada ya Ihefu kukamilisha usajili wa washambuliaji wengine wapya walioingia dirisha dogo la Januari wakiongozwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Mkenya Elvis Rupia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Amza alisema anajisikia furaha kupata changamoto mpya ingawa ana kazi kubwa ya kufanya ndani ya timu hiyo.
“Nakiri msimu huu haujakuwa mzuri kwangu ila bado haujaisha na nina uwezo wa kufanya makubwa kwa muda uliobakia kuanzia sasa, naamini katika kupambana hivyo licha ya kutoanza vyema lakini sijakata tamaa kwani nimezidi kuimarika,” alisema.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema usajili wa mshambuliaji huyo utasaidia kikosini kwa kushirikiana na nyota wenzake huku akisistiza kuwa ni mbadala sahihi wa Anuary Jabir aliyejiunga na Dodoma Jiji.
Akiwa na Ihefu msimu huu, nyota huyo alifunga bao moja la ligi ambalo aliifunga Kagera Sugar Agosti 19, mwaka jana akikumbukwa zaidi msimu uliopita alipofunga mabao saba akiichezea Coastal Union.