Timu ya Ruvu Shooting yenye maskani yake Mlandizi Mkoani Pwani imesema haina mpango wa kuachana na kocha wake, Mbwana Makata licha ya kushindwa kuinusuru na janga la kushuka daraja msimu huu.
Akizungumza jijini Dar es salaam msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire amesema mara baada ya timu hiyo kushuka daraja na kuelekea championship, bado wanaimani na kocha huyo kuendelea kuwatumikia maafande hao, labda kama ataomba mwenyewe kuondoka.
“Itategemea na kocha mwenyewe kama ataridhia kuondoka au kubaki, lakini sisi hatuna tatizo, akiamua kuondoka tutamruhu,” amesema Bwire.
“Ruvu haina tabia ya kumtupia lawama mwalimu inapotea timu imefanya vibaya kwani huwa hatuna kasumba ya kusema mwalimu ndo kasababisha timu kuwa na kiwango kibovu, huwa tuna wigo mpana wa kutafakari mambo mbalimbali na kutafakari wapi tumeteleza na wapi tufanye maboresho ili timu yetu iwe vizuri.”