Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge: Yanga hii inatoboa CAF

Yanga Beki.jpeg Wachezaji wa Kikosi cha Yanga

Mon, 3 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa timu ya Bunge (Bunge SC), Ahmed Juma Ngwali amekiangalia kikosi cha sasa cha Yanga kisha akatamka kibabe kwamba kama wataamua kukaza watatoboa kiulaini tu katika michuano ya CAF na hata Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ngwali ambaye ni mbunge wa Wawi, anayemiliki Leseni B ya ukocha wa soka, huku akiwa amewahi kuichezea timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, alisema amekifuatilia kikosi cha Yanga kwa msimu huu na kuona kina mabadiliko makubwa tofauti na msimu uliopita.

Alisema kwa hali hiyo anaamini kama kitakaza msuli hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, basi kina nafasi ya kufanya vizuri zaidi kulinganisha na msimu uliopita kilipokwama raundi ya kwanza kwa kutolewa na Rivers United ya Nigeria iliyoifumua nje ndani kwa bao 1-0 kila mchezo.

“Naiona Yanga ikifika mbali sana. Kwa sasa inacheza kitimu zaidi na ina wachezaji wenye viwango bora na wa kuamua mechi, hivyo naamini itatetea tena ubingwa wa Ligi Kuu na hata kwenye mechi za CAF ikikomaa ina nafasi kubwa ya kutinga makundi,” alisema mbunge huyo aliyewahi kuichezea Machomanne kwa misimu 10 mfululizo.

Mbunge na kocha huyo, alisema kombinesheni ya Stephane Aziz Ki, Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Fei Toto’ imeibadilisha Yanga na kuifanya iwe inatengeneza nafasi nyingi za kufunga katika mchezo.

Alisema kikosi hicho kimeimarika zaidi kulinganisha na cha msimu uliopita kilichobeba mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC pamoja na kunyakua Ngao ya Jamii iliyoitetea tena msimu huu.

Yanga chini ya Kocha Nasreddine Nabi, imecheza mechi 41 za Ligi Kuu bila kupoteza.

Chanzo: Mwanaspoti