Aina ya uchezaji wa mabeki Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Shomari Kibwana, Bakari Mwamnyeto na Yassin Mustapha (Yanga), umetajwa kuleta uwiano wa thamani sawa wa wageni.
Staa wa zamani wa Yanga, Fredy Mbuna ambaye kwa sasa ni kocha wa Yanga B, aliwataja mastaa hao namna walivyojipambanua kulipa heshima soka kwa matendo nalo linawaheshimisha mbele ya wapenzi wa mpira ndani na nje.
Sababu kubwa iliyomfanya Mbuna, abarikiwe na huduma ya mastaa hao ni ukubwa wa majina yao yanavyoendana na kazi wanayofanya uwanjani, huku wakiwa nguzo muhimu kwenye timu yao ya taifa ‘Taifa Stars’.
“Wakikosekana pengo lao linakuwa wazi, huoni wakirizika na sifa walizonazo mbele ya mashabiki wao, hilo ni jambo la kuigwa na wenzao, kutambua wamefuata kitu gani kwenye soka ambalo halina njia za mkato.” alisema Mbuna na kuongeza.” alisema.
Aliuchambua aina ya uchezaji wa Tshabalala kwamba ni wa kutumia akili zaidi, kujua namna ya kufika mbele kushambuliaji na kuokoa hatari bila kugongana na wapinzani wake.
“Kifupi wapo vizuri sana, ila niwakati wao wa kutoka nje ili wakapate ufahamu mpana zaidi, utakaokuwa msaada kwa Stars.”alisema.
Hoja yake iliungwa mkono na beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah aliyesema anakoshwa na Tshabalala, huku akimpa tahadhari na ujio wa Farid Mussa namna anavyoweza kumpa chachu wa kuwania nafasi kikosi cha Stars.
“Tshabalala anafanya vizuri sana kwenye nafasi ambayo nimecheza, ila namuona Farid anakuja kwa kasi na akitia bidii anaweza akabadilisha upepo wa namba mbele ya Tshabalala kwenye kikosi cha Stars.”alisema.