Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema kutokana na hali ngumu waliyonayo katika Kundi C la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, wanahitaji kupambana kufa au kupona kuhakikisha wanapata ushindi mchezo wao ujao dhidi ya Vipers FC.
Simba itavaana na Vipers ugenini nchini Uganda katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka kufungwa na Horoya, kisha Raja Casablanca.
Timu hiyo, hadi hivi sasa haijapata pointi ikiburuza mkia wa Kundi C baada ya kufungwa 1-0 dhidi ya Horoya, kisha nyumbani ikachapwa 0-3 na Raja Casablanca.
Akizungumza nasiRobertinho alisema hawatakiwi kupoteza mchezo wowote kati ya minne waliyoibakisha katika kundi lao, wakianza na Vipers.
Robertinho alisema anaamini wakipata ushindi dhidi ya Vipers matumaini na malengo ya kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika yatakuwepo.
Aliongeza kuwa, anaendelea kukiboresha kikosi chake katika kila eneo ikiwemo ulinzi ambayo iliruhusu mabao mengi dhidi ya Raja Casablanca pamoja na ushambuliaji inayoshindwa kutumia nafasi za kufunga.
“Kulingana na hali yetu ilivyo kwenye kundi, tunahitaji kwenda Uganda kushinda dhidi ya Vipers, sio kazi rahisi lakini tutajitahidi kupambana.
“Kama tukifanikiwa kupata ushindi na Vipers malengo yetu ya kufuzu hatua ya robo fainali yatakuwa kwenye hali nzuri.
“Uzuri zaidi kwangu ninawafahamu vizuri Vipers kwani niliwahi kuifundisha, hivyo nitakiboresha kikosi changu kwa kuwapa mbinu nzuri za ushindi,” alisema Robertinho.