Kiungo Mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes amemchongea Aishi Manula kwa wadau wa soka baada ya kuibuka baadhi wakimtetea na kumbukusha anapaswa kujitafakari kutokana na kujisahau anapokuwa langoni.
Gomes ambaye ni Mbrazili alimtungua Manula kwa mpira wa friikikii wikiendi iliyopita wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara na Simba ilishinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza kipa wa zamani wa kimataifa aliyezidakia Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, Majimaji na Taifa Stars, Steven Nemes alisema ni kama vile Manula amebweteka sana ndio maana timu hiyo imeyumba kwenye ulinzi na inaruhusu mabao mfululizo huku akisisitiza kuwa ni kipa mzuri anatakiwa kujitambua.
Alisema amecheza ndani ya miaka mitano kwa mfululizo, tangu yupo Azam FC na sasa Simba, hilo limethibitisha ubora wake kinachomuangusha ni kukosa changamoto ya kumpa ushindani anajisahau na kujikuta anajiamini sana.
“Sina maana kwamba Beno Kakolanya ni mbaya kinachotakiwa ni kumpa nafasi ya kucheza ili kumuamsha Aishi ambaye anajua kila mchezo ni lazima acheze kutokana na kujitengenezea nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema Nemes na kuongeza;
“Nafurahishwa na uwezo wake akiwa kwenye ubora kwa mechi za hivi karibuni ukiachana na bao la Gomes ambalo hapaswi kulaumiwa amekuwa akiruhusu mabao mepesi sana hasa mechi na Tanzania Prisons anatakiwa kuliangalia hilo ili aendelee kujitengenezea mazingira mazuri ya kuwa bora zaidi.”
Kocha wa makipa aliyewahi kuinoa Simba, Idd Pazi ‘Father’ alimchambua Manula kwamba kadri anavyocheza ndivyo anamuona anazidi kuwa bora, ingawa alienda mbali kwamba anahitaji mshindani ambaye anaweza kumuweka benchi.
“Angalau Beno Kakolanya ndiye kipa niliyekuona anakuja kushindania namba moja na Manula, lakini naye amekubali kukaa benchi na kumsubiri kipa huyo anapopata shida ndio acheze hilo linamlemaza hatakiwi kufikia huko anatakiwa kucheza akiamini akikosea kuna mtu anachukua namba yake.”
“Ili mchezaji awe na uzoefu lazima awe anacheza mechi nyingi kama ilivyo kwa Aishi lakini naona ameanza kuwa na shida hii inatokana na kukosa mshindani anafanya makosa ambayo kwa ubora wake na uzoefu hatukutarajia.”
Bao la Bruno ni kati ya mabao ambayo kwa msimu huu yamekuwa yakimtesa Manula, likiwamo alilotunguliwa na Stephane Aziz KI katika mechi ya Kariakoo Derby iliyoisha kwa sare ya 1-1.