Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbrazili ajipange kwa Manula

Caique Luizt Santos Da Purificacao.jpeg Mbrazili ajipange kwa Manula

Wed, 12 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni zamu ya Mbrazili Caique Luiz Santos da Purificao kutafuna mfupa uliowashinda wengi tangu Simba ilipomsajili Aishi Manula kutoka Azam FC.

Manula amedhihirisha kweli ni kipa anayestahili kusimama kwenye milingoti mitatu ya goli akiwa na Taifa Stars na klabu yake ya Simba. Hana mpinzani.

Safari yake ya soka ni tamu, amecheza mechi nyingi tangu akiwa Azam FC na kuipa mafanikio kabla ya kumwaga wino kwa Wekundu wa Msimbazi na kuonyesha kweli mabosi wa timu hiyo hawakufanya kosa kumsajili.

Alitua Simba msimu wa 2017/18 akichukua nafasi ya Mghana, Daniel Agyei na tangu hapo ameibuka kuwa shujaa sio tu kwenye Ligi Kuu Bara bali hata kwenye michuano ya kimataifa Simba ikishiriki kwa misimu mitatu mfululizo na huu ukiwa wa nne wakienda tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf Champions League).

Wamepita makipa wengi ndani ya Simba na wameonyesha uwezo wao lakini ni dhahiri kwa Manula hakuna anayemfikia.

Achana na ubora wa kikosi cha Simba hasa kuanzia eneo la beki hadi washambuliaji lakini Manula anafichua kilichomfanya awe bora tangu alipoaminiwa na kusajiliwa na kupewa jukumu la kulinda milingoti mitatu ya mabingwa hao mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara waliofika hatua ya robo fainali mara mbili mfululizo na kuweka heshima kwenye michuano ya kimataifa kuwa ni kuamini katika upambanaji.

Tangu atue Simba, Manula ameiwezesha kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni misimu minne mfululizo.

Pia ameisaida kubeba taji la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara mbili mfululizo na ana tuzo kibao binafsi kama ya kipa bora.

Kwa upande wa michuano ya kimataifa ameifikisha Simba hatua ya robo fainali mara mbili mfululizo na kuchaguliwa kwenye kikosi cha michuano hiyo walipotinga hatua hiyo.

Hapa tunakuletea makipa waliopita chini ya Manula na kushindwa kufanya vyema kwa kumpa ushindani kwenye kikosi hicho ambacho amejijengea ufalme wa kuwa kipa namba moja.

BENO KAKOLANYA Alitua Simba akitokea Yanga msimu wa 2019 wadau wa soka wengi walitarajia ushindani wa namba kwa wawili hao lakini haikuwa hivyo.

Kakolanya ameitumikia Simba misimu minne lakini hakumpa changamoto Manula kwani alikuwa anapata nafasi ya kucheza pale ambapo kipa namba moja anapokuwa na shida Kipa huyo ambaye inasemekana kamalizana na Singida Fountain Gate akiwa Simba ametwaa mataji matatu na kucheza hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

SAID MOHAMED 'NDUDA' Said Mohamed 'Nduda' alijiunga Simba akitokea Mtibwa Sugar aliwahi kuzidakia Majimaji na Yanga kabla ya kuibukia Mtibwa.

Kipa huyo ambaye aliwahi kutwaa tuzo ya kipa bora akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars katika michuano ya COSAFA huko Afrika Kusini, alikutana na upinzani mkali ndani ya Simba kutoka kwa makipa waliosajiliwa wakati huo ambao ni Manula na Emmanuel Mseja kutoka Mbao FC. Baadaye Nduda aliamua kutimkia Ndanda FC.

DEOGRATIUS MUNISHI 'DIDA' 2018 ulikuwa ni msimu wake wa pili kurudi tena Simba alitokea Afrika Kusini, Dida alikuwa anaichezea Klabu ya Chuo Kikuu cha Pretoria 'Tucks FC'.

Ujio wake ndani ya Simba uliwaaminisha wadau wengi wa soka kuwa atampa ushindani Manula kutokana na uzoefu wake na ubora aliokuwa nao lakini hakufanya hivyo kwani alidumu msimu mmoja na baadaye kutimliwa.

Dida mchezaji wa zamani wa kikosi hicho ingawa alizichezea pia Yanga, Mtibwa Sugar na Azam FC miaka ya nyuma kabla ya kutimkia Afrika Kusini.

EMMANUEL MSEJA Mseja ni miongoni mwa wachezaji ambao walisajiliwa Simba na analipwa mshahara wake kama kawaida lakini hakuwa kwenye programu ya kocha, Mbelgiji Patrick Aussems kipindi hicho anasajiliwa.

Ni usajili ambao uliwashangaza wengi alisajiliwa akitokea Mbao FC pamoja na Nduda ambaye alijiunga na kikosi hicho na kutambulishwa kama mchezaji wa Simba.

Kipa huyo pia aliachwa kwenye ziara ya Simba nchini Uturuki ilipoenda kuweka kambi na hakutambulishwa kwenye Simba Day kama mmoja ya wachezaji wa msimu huo.

Swali ni je, Mbrazili Purificao ambaye anatajwa kumalizana na Simba na kutarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia sasa anaweza kumudu mikikimikiki ya Manula ambaye yupo nje ya uwanja kwa kuuguza majeruhi.

Manula amefanyiwa upasuaji wa nyonga na kushindwa kumalizia mechi za ligi na Kombe la Shirikisho Afrika atakuwa nje hadi mwanzo wa msimu ujao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: