Kiungo mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes amefichua uhusiano uliopo baina ya rafiki yake aitwae, Samuel baada ya kumuandikia ujumbe wa maandishi wakati alipoifungia timu yake bao moja katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Liti Singida, Bruno alionyesha tisheti yake ya ndani ambayo iliyokuwa na ujumbe uliosomeka “Pumzika kwa amani. Nitakupenda milele ndugu yangu Samuel,” akikienzi kifo cha rafiki yake huyo kilichotokea huko Brazil.
Akizungumza baada ya maneno hayo, Bruno alisema alitamani sana kufunga kwenye mchezo huo ili kutoa zawadi kwa rafiki yake Samuel ambaye amekuwa naye bega kwa bega katika kumsapoti na kumtia moyo kwenye kila hatua anayopiga.
“Ni rafiki ambaye nitamkumbuka sana kwa sababu wakati natoka Brazili aliniambia kwa kipaji nilichonacho nitafanya vizuri huku niendako licha ya ugeni wangu na mazingira tofauti niliyozoea, kiukweli nitamkumbuka sana,” alisema na kuongeza;
“Mwanzoni ilikuwa vigumu sana kuamini kama ninaweza kutoka sehemu moja na kwenda nyingine nikacheza kama hivi kwa sababu mazingira ambayo nilitoka na huku ni tofauti ingawa yeye alisimama na kuniambia Bruno ondoa wasiwasi kaka unaweza.”
Kuhusu muendelezo mzuri wa kiwango chake, Bruno alisema ushirikiano ndio silaha kubwa ya kufanya vizuri kwani bila ya jitihada za wachezaji wenzake asingeweza kufanya chochote hivyo anashukuru benchi la ufundi kwa kuendelea kumuamini.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu amekuwa mchezaji tegemeo chini ya Kocha Hans van der Pluijm na katika michezo 20 aliyocheza hadi sasa amefunga mabao saba akiwa ndiye anayeongoza nyuma ya mshambuliaji, Meddie Kagere mwenye mabao matano.