Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ anawasoma wapinzani wake, Power Dynamos ya Zambia huku jina la kwanza kwake kulifuatilia likiwa ni kiungo wa kati, Joshua Mutale.
Timu hizo zinakutana Septemba 16 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa katika mchezo wa raundi ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuwania kufuzu hatua ya makundi itakayoanza Novemba mwaka huu.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Robertinho alisema lengo ni kuwatambua vyema wapinzani hao huku akikiri anahitaji kumaliza mchezo huo ugenini.
“Tunaenda kwenye michuano mikubwa Afrika hivyo ni lazima tujiandae vizuri kwa maana ya kiakili na kimwili, wapinzani wetu wana wachezaji wazuri ila Mutale ni hatari zaidi,” alisema.
Robertinho aliongeza licha ya ubora wa nyota huyo ila jukumu kubwa ni kupambana na timu nzima, kwani kwa kufanya hivyo itawapa nafasi ya kuepuka mtego wa kumtegemea zaidi mchezaji mmoja tu.
“Kila timu ina mchezaji wake tegemeo lakini tunachoenda kufanya ni kukata mawasiliano kati yake na wenzake, hii itatusaidia kwa sababu Mutale ni mzuri kwenye kuanzisha mashambulizi,” alisema.
Dynamos ilifuzu hatua hiyo kwa bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza kupoteza mabao 2-1 dhidi ya African Stars ya Namibia kisha marudiano ikiwa kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa kushinda 1-0.
Mchezo wa mwisho kwa timu hizi kukutana ulipigwa Agosti 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika kilele cha Simba Day ambapo Simba ilishinda mabao 2-0.
Tangu Simba iliposhinda mabao 5-0 dhidi ya Mufulira Wanderers katika michuano ya ubingwa wa Afrika mwaka 1979 haijawahi kushinda tena hadi leo kwenye ardhi ya Zambia.