Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewapa matumaini wachezaji na viongozi wa Yanga kwa kushindwa kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
Yanga jana usiku ilikuwa Uwanja wa Stade du 5 Juillet kucheza mechi ya pili fainali CAFCC dhidi ya USM Alger na mshindi alipatikana kwa sharia ya mabao ya ugenini na nyumbani ambapo USMA walishinda mechi ya kwanza ugenini mabao 2-1 na jana Yanga ilishinda bao 1-0 ambalo halikuweza kuwafanya kuwa mabingwa.
Kupitia mitandao ya kijamii rasmi anayotumia Mbowe ameandika; “Mimi ni muumini wa kutokukata tamaa, ni muumini mzuri pia wa kupambania ninachokiamini kwa gharama yoyote, na ndicho Yanga mlichokionyesha jana,”
“Asanteni kwa hili, pongezi za dhati kwa kuweka alama kwenye mashindano ya kimataifa ya CAFCC, sina shaka wakati ujao tutalibeba kabisa kombe. Pongezi za dhati kwa wachezaji, benchi la ufundi, uongozi wa klabu na mashabiki kwa kujitoa kwenu kwa hali na mali. Mmeliheshimisha Taifa,”