Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbongo ahitimu ukocha alikosoma Ferguson na Mourinho

Mbongo Ukocha Mbongo ahitimu ukocha alikosoma Ferguson na Mourinho

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mtanzania Emanuel Saakai ametunukiwa leseni A ya UEFA na chama cha soka huko Scotland ambako walinolewa makocha mbalimbali wakubwa barani Ulaya akiwemo Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho na Arrigo Sacchi.

Saakai ambaye ndoto yake ni kuifundisha Taifa Stars, alihitimu mafunzo hayo siku chache zilizopita chini ya mkufunzi Jack Ross ambaye ni kocha wa zamani wa St Mirren, Dundee United, Hibernian, na Sunderland.

Kwa sasa Ross ni mkuu wa kitengo cha maendeleo ya makocha katika klabu ya Newcastle United inayoshiriki Ligi Kuu England.

Akiwa mwenye furaha baada ya safari ndefu ya kujiendeleza, Saakai alisema, “Hakika hakuna jambo linaloshindikana chini ya jua, ukiamini na kuweka nia unaweza kufanya mambo mengi makubwa ambayo kikawaida unaweza kuona ni ngumu kufanyika.”

“Sijacheza soka kwenye kiwango kikubwa cha ushindani lakini leo nimebahatika kupata leseni A ya Uefa, nitoe shukrani kwa wote ambao wamekuwa sehemu ya safari yangu, sasa ni muda wa kufanya kazi.”

Kuhusu kusoma pahali ambako wamepita makocha wengi wakubwa kwenye soka la Ulaya, Saakai ambaye ni Mmasai alisema kwake ni bahati na anachoshukuru Mungu zaidi ni namna alivyokuwa akipata usaidizi kutoka kwa Ross ambaye ni mmoja wa wakufunzi waliokuwa naye kwa karibu.

“Kiukweli ni mtu poa sana ambaye anatamani kuona nikifanya makubwa kutokana na hiki nilochokipata, najua ni ngumu kupata kazi kwenye timu kubwa lakini nina nafasi ya kuanzia chini na kuonyesha uwezo wangu hadi kufika hatua kubwa zaidi,” alisema kocha huyo.

Saakai wakati akijitafuta aliwahi kufanya kazi ya kufundisha kwenye vituo mbalimbali vya soka ikiwa ni pamoja na kituo cha nyota wa zamani wa Liverpool, Harry Kewell, pia amefanya kazi na akademi za FC Barcelona na Juventus huko Australia ambako makazi yake ndipo yaliko.

Mtanzania huyo amepigwa msasa katika semina mbalimbali ambazo ziliandaliwa kwa nyakati tofauti na FC Barcelona, Manchester City, Cardiff City, Ajax, Juventus, Scottish FA, FA ya Italia (FIGC), Ubelgiji FA (RBFA), FA ya Ujerumani (DFB), Welsh FA (FAW).

Chanzo: Mwanaspoti