Mshambuliaji wa Azam FC, Idriss Mbombo ameihakikishia timu yake pointi tatu muhimu na kuvunja uteja kwa Mbeya City baada ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu NBC uliopigwa katika uwanja wa Sokoine.
Ushindi huo unaifanya timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa pointi nane, zaidi ikiwa ni kulipa kisasi kwa wapinzani hao ambao msimu uliopita waliitesa kwa kuchukua kwao pointi nne.
Katika mchezo huo timu zote zilicheza soka safi kwa kila upande kuweka mipango yake lakini ilishuhudiwa dakika 45 za kwanza zikimalizika bila kufungana.
Hata hivyo katika muda huo timu zote zingeweza kwenda mapumziko kwa mabao lakini umaliziaji ulikuwa butu kwani Mbeya City ilipata nafasi kupitia kwa Joseph Ssemuju dakika ya 33 ila mipira yake haikuwa na macho.
Kadharika upande wa Azam walipata nafasi kadhaa, lakini mashuti yao yaliishia miguuni mwa mabeki wa City mengine Kipa Haroun Mandanda akiyadaka kiuwepesi.
Kipindi cha pili kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdalah Mubiru aliwapumzisha Ssemuju na George Sangija na kuingizwa Eliud Ambokile na Gasper Mwaipasi, hali iliyowapa wakati mgumu mabeki wa Azam.
Azam ilifanikiwa kupata bao la uongozi na la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake Idriss Mbombo dakika ya 61 baada ya wachezaji wa City, Ambokile na Samson Madeleke kupasiana mpira na kumkuta mfungaji aliyejikokota nao na kumchungulia Kipa na kuujaza wavuni.
Mbeya City waliamka na kulazimisha mashambulizi lakini mlango wa Azam ulikuwa mgumu kupenyeza mipira kutokana na mashuti mawili kugonga nguzo ikiwamo ya Mwaipasi dakika ya 74 Nelson Ruta dakika ya 79.
Mchezaji Rodgers Kola alijikuta akioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi Ramadhan Kayoko dakika ya 90 kwa kumchezea rafu kipa wa Mbeya City, Mandanda.