Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya Kwanza yachukua wawili kimataifa

Meya Kwanza Kimataifa Mbeya Kwanza yachukua wawili kimataifa

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pointi 32 walizovuna Mbeya Kwanza zimewapa matumaini benchi la ufundi likianza kupiga hesabu za raundi ya pili kwa ajili ya kurejea Ligi Kuu, huku ikiweka wazi usajili wa nyota kutoka Ghana na Nigeria.

Timu hiyo iliyowahi kucheza Ligi Kuu msimu wa 2020/21 na kushuka daraja, imeweka kambi yake mkoani Mtwara kwenye Championship na imekuwa na matokeo mazuri kuwapa matumaini mashabiki kurejea tena.

Katika mzunguko wa kwanza timu hiyo imemaliza nafasi ya pili kwa alama 32, licha ya kuwa imeondokewa na staa wake, Ramadhan Kapera (Geita Gold) na aliyekuwa kocha mkuu, Maka Mwalwisi aliyejiunga na TMA FC.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Michael Mnyali alisema malengo yao hayajatimia kwani hesabu zilikuwa ni kumaliza mzunguko wa kwanza kwa pointi 36 kileleni lakini hata walichopata si haba.

Alisema wanaenda kujipanga raundi ya pili wakiboresha kikosi kwa usajili wa mastaa sita na hadi sasa tayari wamemalizana na nyota wawili, huku wanne wakiwamo wa kigeni wakisubiri kukamilika kwa vibali vyao.

“Ambao ni tayari ni Tau Salum (Ruvu Shooting), Yusuph Idd kutoka Pan Africa na wengine wanne wakiwamo Mghana na Mnigeria muda wowote tutamalizana nao baada ya kukamilisha vibali,” alisema Mnyali.

Kocha huyo aliongeza kuwa hesabu zao ni kurejea Ligi Kuu akikiri kuwa upinzani uliopo kwenye Championship unawapa akili kubwa kuendelea kupambana kutoshuka nafasi mbili za juu.

“Ingekuwa rahisi tusingekuwa tunafanya usajili au maandalizi yoyote, lakini tunashukuru vijana nao ni wapambanaji na mipango ni ile ile kurejea tulipokuwa,” alisema kocha huyo.

Chanzo: Mwanaspoti