Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya Kwanza mambo mazito

Mbeya Kwanza Pic Mbeya Kwanza yaqkubali kichapo nyumbani

Fri, 17 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mzimu wa matokeo mabaya katika uwanja wa Sokoine umeendelea kuisumbua Mbeya Kwanza baada ya leo kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Namungo.

Mchezo huo unakuwa wa sita kwa Mbeya Kwanza kupoteza katika Ligi Kuu ikiwa ni sare nne na vichapo viwili na kuamsha presha kwa mashabiki katika vita ya kushuka daraja.

Namungo ilipata bao pekee lililoipa pointi tatu kupitia kwa winga wake, Reliant Lusajo dakika ya tisa na kutosha kabisa kumaliza mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko ambapo Namungo iliwatoa Obrey Chirwa na Abdulmarick Adam na nafasi zao kuchukuliwa na Daniel Joram na David Moringa huku Mbeya Kwanza wakimtoa William Edgar na Chesco Mwasimba na nafasi zao kujazwa na Hamis Kanduru na Mohamed Rashid.

Mabadiliko hayo yaliifanya Namungo kutuliza mpira na kuanza kushambulia kwa kushtukiza huku Moringa na Kichuya wakikosa nafasi kadhaa za wazi huku Kipa wa Mbeya Kwanza, Hamad Kadedi kufanya kazi ya ziada kwa kuokoa michomo ya nyota hao kwa dakika tofauti.

Mbeya Kwanza walipambana kusawazisha bao hilo lakini walikutana na ulinzi imara chini ya beki, Baraka Mtuwi na Kipa wao, Jonathan Nahimana.

Kwa matokeo hayo, Namungo wanafikisha pointi 12, huku Mbeya Kwanza wakibaki na alama zao saba na kuendelea kubaki nafasi za mkiani.

Katika mchezo huo baadhi ya viongozi kutoka shirikisho la soka nchini (TFF) walishuhudia kandanda hiyo akiwamo Katibu Mkuu, Wilfred Kidao sambamba na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Mhandisi, Heris Said na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya, (Mrefa).

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz