Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya Derby kitawaka leo

Ihefu Warm Up.jpeg Mbeya Derby kitawaka leo

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kitawaka. Ndivyo unaweza kusema pale Ihefu na Tanzania Prisons zitakapokutana leo Jumatatu kwenye mchezo wa Ligi Kuu kuwania pointi tatu, huku makocha wote wakisisitiza kuwa lazima kitaeleweka.

Timu hizo za jijini hapa zinatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Highland Estate kila upande ukihitaji pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo kutokana na matokeo yasiyoridhisha.

Kibarua zaidi kitakuwa kwa kocha mkuu wa Ihefu, Moses Basena ambaye tangu ametambulishwa kikosini mapema Oktoba hajaonja ushindi wowote kwenye michezo sita aliyosimamia.

Katika mechi hizo, Ihefu imepoteza michezo minne dhidi ya Simba 2-1, KMC 1-0, Azam 3-1 na Namungo 2-0, huku ikitoa sare mbili mbele ya Singida Big Stars 2-2 na JKT Tanzania 1-1 na kuwa nafasi ya 14 kwa pointi tisa.

Kwa upande wa Prisons ambao walisotea ushindi kwa siku 52 tayari kocha wake mkuu, Ahmad Ally ameanza kwa kishindo alipoipa pointi tatu timu hiyo kwenye mechi iliyopita dhidi ya Dodoma Jiji na kukaa katika nafasi ya 13 kwa alama 10.

Basena alisema mchezo huo ni muhimu sana na baada ya kusota kwa muda mrefu bila ushindi sasa wanasubiri kuanza kazi rasmi leo akiwataka nyota wake kukomaa kuibuka na ushindi.

“Tumejipanga, tunajua kila mmoja anataka ushindi ila sisi ndio wahitaji zaidi na matarajio yangu ni kushinda mechi hiyo na kujiweka pazuri kwenye msimamo,” alisema kocha huyo raia wa Uganda.

Naye kocha wa Prisons, Ally alisema matokeo aliyoanza nayo kwa mara ya kwanza tangu kukabidhiwa kikosi hicho, yametoa mwanga na matumaini kuhakikisha wanaendeleza ushindi.

“Tunaenda kupambana kwa sababu tunafahamu hata wapinzani hawako pazuri, ari na morali kwa vijana ni kubwa na matumaini yetu ni kuendeleza ushindi ili kujinasua nafasi za chini,” alisema kocha huyo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: