Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City yaifuata Singida Big Stars mapema

Ruvu Shootinga Vs Mbeya Mbeya City yaifuata Singida Big Stars mapema

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Mbeya City kinatarajia kuondoka leo jijini Mbeya kwenda Singida kwa ajili ya mchezo wa robo fainali Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) dhidi ya Singida Big Stars.

Mchezo huo utapigwa mwishoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Liti na katika mchezo wa Ligi Kuu zilipokutana kwenye uwanja huo Agosti 20 mwaka jana, Mbeya City ilikufa kwa mabao 2-1.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mbeya City kufika hatua ya robo fainali tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013/14, chini ya Kocha Juma Mwambusi.

Mbeya City imefika hatua hiyo baada ya kuichapa Stand FC ya Mtwara mabao 5-1 hatua ya 32 kisha ikiichapa Kagera Sugar bao 1-0 Uwanja wa Kaitaba hatua ya 1.

Msimu uliopita Mbeya City ilitolewa hatua ya kwanza na African Lyon kwa penalti 4-3 baada ya sare ya mabao 2-2 na mara ya mwisho kukutana na Singida Uwanja wa Liti ilikuwa Agosti 20, mwaka jana na Mbeya City kuchapwa bao 1-0.

Kocha msaidizi wa Mbeya City, Anthon Mwamlima alisema hadi kufika hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwao sababu misimu yote walikuwa wakiishia hatua za awali lakini sasa wapo robo fainali.

Mshindi kati ya Mbeya City na Singida atakutana na mshindi kati ya Yanga na Geita Gold Uwanja wa Liti wakati mshindi kati ya Simba na Ihefu atacheza na mshindi kati ya Azam na Mtibwa katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Katibu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe alisema moja ya lengo walilokuwa wameliweka msimu huu kwenye Ligi Kuu ni kumaliza ‘top four’ ambayo ingewasaidia kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Alisema kwa hesabu ya michezo iliyosalia kwenye ligi na nafasi waliyokuwa nayo hivi sasa, hawaoni kama watafanikiwa kumaliza katika nafasi nne za juu.

“Tunahitaji kwenda fainali safari hii sababu kwenye ligi hatutafikia lengo letu, hivyo tukifanikiwa kuchukua ubingwa tunakuwa tumekata tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Mchezo tunajua utakuwa mgumu sababu wenzetu wapo nyumbani na michezo yote ya ASFC imecheza ikiwa nyumbani tofauti na sisi ambao mchezo uliopita tumecheza ugenini,” alisema Kimbe.

Mbeya City ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi kwa alama 27 huku ikisalia na michezo mitano ambayo ikifanikiwa kushinda michezo yote itafikisha alama 42 wakati Azam inayoshika nafasi ya nne hadi sasa ina alama 47.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live