Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City wasema Yanga hawatoki kesho

33798 Pic+mbeya Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa Mbeya City Ramadhan Nsanzurwimo amesema atakachokifanya kesho, ni kutibua rekodi ya Yanga kutofungwa watakapokutana kesho kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Yanga itakuwa ugenini kesho kuikabili Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara huku ikiwa na rekodi ya kutopoteza mchezo hadi sasa pamoja na Azam.

Hata hivyo, kocha wa Mbeya City, Nsanzurwimo alisema anajua ubora na udhaifu wa Yanga hivyo anaufanyia kazi ili aikamate vizuri timu hiyo na kuhakikisha haifurukuti dhidi yao.

“Tunaendelea na maandalizi yetu na nashukuru wachezaji wangu wote wako vizuri na naomba Mungu wawe salama hivyo hivyo mpaka siku ya mechi.

“Najua ninakutana na timu kubwa, inayooingoza ligi na ambayo haijapoteza mchezo lakini siwaogopi wala siwahofii.

“Yanga nimeifuatilia na kujua wana ubora sehemu gani, nguvu yao iko wapi na maeneo gani ni wabovu, hivyo tutayafanyia kazi hayo yote hayo ”alisema.

Yanga yawasili kibabe Mbeya.

Yanga jana iliondoka alfajiri ya saa 11:30 alfajiri kwa ndege na kutua katika jiji la Mbeya majira ya saa 12:30 asubuhi. Baada ya kufika timu hiyo ikaweka kambi katika hotel ya FQ .

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera naye ameshawasili nchini usiku wa kuamkia jana akitokea Ufaransa na kuunganisha kwenda Mbeya tayari kwa mchezo wa kesho.

Akizungumza baada ya kuwasili,

Zahera aliwashukuru Mashabiki na wanachama wa klabu hiyo walioichangia timu hiyo na kuiwezesha kusafiri kwa ndege kwenda Mbeya huku akiwaahidi kuwapa furaha ya matokeo mazuri uwanjani. Awali Zahera aliwaomba mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuichangia timu ili isafiri kwa ndege kwenda Mbeya na kuwapunguzia uchovu wachezaji huku akiahidi kama hela isingetosha nyingine angeongezea mwenyewe.

“Ninawashukuru sana mashabiki kwa kuichangia timu hivyo ndivyo inavyotakiwa na ninaahidi kuwapa furaha kesho,” alisema.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa Kagera kucheza na JKT Tanzania Uwanja wa Kaitaba Bukoba wakati KMC itaikabili Mbao kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Stand itaivaa Alliance Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mechi za kesho Jumamosi Lipuli itaikaribisha Ndanda kwenye Uwanja wa Samora Iringa na Mwadui itakuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuivaa African Lyon.

Mtibwa Sugar itacheza na Azam kwenye Uwanja wa Manungu Turiani wakati Ruvu Shooting itapambana na Biashara United kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi.



Chanzo: mwananchi.co.tz