Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City chali, Prisons mwendo mdundo

Mbeya City Mbeya city yaaga mashindano

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mbeya City FC imekuwa timu ya kwanza Ligi Kuu kuaga michuano ya kombe la shirikisho (ASFC) baada kupoteza penalti 4-3 dhidi ya African Sports kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

Pia matokeo hayo yanawafanya 'Wanakimanumanu' kutoka jijini Tanga kuwa timu ya kwanza ya Championship kufuzu hatua ya 32 baada ya jana  Jumanne kushuhudia timu saba za ligi hiyo zikiondoshwa.

Hata hivyo matokeo yanakuwa ya kwanza msimu huu kwa Mbeya City kupoteza mchezo katika mashindano yake kwani kabla ya mechi hiyo ilikuwa imeshuka uwanjani mara nane bila kupoteza ikiwa ni sare tano na kushinda mitatu za Ligi Kuu.

Katika mchezo wa leo Jumatano ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa ulikuwa lazima mmoja abaki mwingine asonge katika hatua 32, ambapo Mbeya City ya Ligi Kuu ilijikuta ikiondoshwa dhidi ya wapinzani hao wa Championship.

Katika mchezo huo Mbeya City walionesha soka la kasi wakitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia vyema, huku African Sports wakionesha nidhamu kubwa katika kukaba kushambulia huku Kipa wao, Fikirini Bakari akionesha kiwango kikubwa kwa kuokoa hatari nyingi.

Timu hiyo ilicheza kwa tahadhari kubwa na kushambulia kwa kushtukiza lakini hadi dakika 90 zinamalizika, hakuna aliyeona lango la mwenzake hadi ilipoamuriwa mikwaju ya penalti na African Sports kuibuka na ushindi huo.

Wakati huohuo, Tanzania Prisons wameendelea kutakata baada ya kuwasambaratisha Kitayosce mabao 3-0 katika mwendelezo wa michuano hiyo, mchezo uliopigwa uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

Mabao katika mchezo huo yaliyoifanya timu hiyo kufuzu hatua ya 32, yaliwekwa wavuni na Jumanne Elfadhir, Julius Kangwa na Samson Mbangula.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz