Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City, Ihefu hakuna mbabe

Ihefu Pic Bb Mbeya City, Ihefu hakuna mbabe

Sat, 8 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mbeya City na Ihefu zimeshindwa kutambiana katika mchezo wa Ligi Kuu baada ya kulazimishana sare ya bao 1-1 ikiwa ni mechi ya pili mfululizo kwa timu hizo zikipata matokeo hayo.

City katika mechi iliyopita walitoshana nguvu ya 2-2 na Mtibwa Sugar huku Ihefu ikikamuana na Prisons 1-1.

Katika mchezo wa leo Jumamosi, Mbeya City walianza kwa kasi kwa takribani dakika 10 wakimiliki mpira na kuwafanya kupata bao la mapema kupitia kwa kinara wao wa mabao, Sixtus Sabilo dakika ya tatu na kufikisha mabao matatu na kuwachanganya wapinzani Ihefu.

Hata hivyo Ihefu nao hawakuonesha unyonge kwa wakilazimisha mashambulizi na dakika ya 11 Jafari Kibaya kuisawazishia bao na kufikisha mabao mawili ikiwa ni mechi ya pili mfululizo akitupia wavuni baada ya ile dhidi ya Prisons waliyotoa sare ya 1-1.

Katika mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, timu zote zilicheza kwa tahadhari na mashambulizi ya kushtukiza huku rafu za hapa na pale zikichezwa na pande zote.

Pamoja na timu hizo kutengeneza nafasi lakini umakini kwa Straika wake ulikuwa mdogo kwa kushindwa kumalizia mipira ya mwisho hususani kwa Ihefu.

Licha ya kwenda mapumziko kwa nguvu sawa ya kufungana bao 1-1, lakini Ihefu itajilaumu zaidi kutokana na kushindwa kufunga mabao kwani hata kona tatu walizopata dhidi ya moja kwa City pamoja na mipira ya faulo haikuwa na faida kwao.

Wachezaji Never Tigere aliyedundisha mpira wakati mwamuzi Nassoro Mwinchui amepuliza kipyenga, Samuel Onditi aliyemchezea rafu Eradius Salvatore wa Mbeya City na Papy Tshishimbi wote wa Ihefu walijikuta wakioneshwa kadi ya njano katika dakika ya 43, 58 na 63.

Dakika ya 64 City walimpumzisha Joseph Ssemuju na Sabilo kuwaingiza Gasper Mwaipasi na Eliud Ambokile, huku Ihefu ikiwatoa Tigere, Tshishimbi na Kibaya na nafasi zao kujazwa na Evaligestus Mujwahuki, Godfrey Kitenga na Obrey Chirwa.

Pamoja na mabadiliko hayo, hayakubadili matokeo na kufanya dakika 90 kuisha kwa sare hiyo na kuwafanya Ihefu kubaki mkiani kwa pointi mbili na michezo sita huku Mbeya City wakifikisha pointi sita baada ya michezo saba.

Chanzo: Mwanaspoti