Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City: Hakuna mchezaji anayedai

F6e92783 4d00 4c64 A4eb 71160440e8a4.jpeg Mbeya City: Hakuna mchezaji anayedai

Thu, 18 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Mbeya City umekanusha vikali taarifa za kudaiwa na wachezaji ikielezwa ndio chanzo cha timu hiyo kutopata matokeo mazuri huku ukiweka wazi mipango yao ya kubakiza ligi kuu.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 18, wakati wa hafla ya uzinduzi wa hamasa kwa mashabiki, Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema taarifa zilizosambaa zikieleza wachezaji wa City kudai mishahara si sahihi.

Amesema uongozi hadi sasa umeshalipa kila kitu ikiwamo bonasi za mechi zilizopita na sasa wanachopambania ni kuhakikisha mechi mbili zilizobaki wanapata ushindi wakianza na Yanga, Mei 24.

Amesema katika kupambania timu hiyo kubaki ligi kuu, wamekuwa wakihangaika sehemu tofauti kutafuta wadau kuwezesha kiuchumi ili kufikia malengo yao huku na kwamba muitikio umekuwa mzuri.

“Taarifa hizo tumezisia lakini niwahakikishie kuwa hakuna mchezaji anayedai timu hadi sasa, tumelipa hadi bonasi za kila mechi kulingana na makubaliano, tunaendelea kujipanga kushinda mechi hizi zilizobaki,” amesema Issa.

Kwa upande wake afisa habari wa Taasisi ya Tulia Trust, Addy Kalinjira amesema katika kuhamasisha wadau na mashabiki wa timu hiyo kuipenda Mbeya City na kujitokeza katika mechi ijayo dhidi ya Yanga, watagawa jezi bure.

Amesema zoezi la kugawa jezi za Mbeya City kwa mashabiki linaanza leo ambapo jezi 1,000 zitagawiwa katika kata 36 za jiji la Mbeya na kuwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kwenye mechi ya Mei 24 kwenye uwanja wa Sokoine.

“Tunafanya hivi kwa maelekezo ya spika wa bunge, Dk Tulia Ackson ambaye ni mkurugenzi wa taasisi hii na mbunge wa Mbeya mjini, lakini amekuwa mdau wa soka na Mbeya City hivyo tujitokeze kuishangilia timu yetu,” amesema Kalinjila.

Chanzo: Mwanaspoti