Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji kuwatumia ‘marizevu’ kuwavaa KMC

32391 PIC+SIMBA Simba

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada Simba kupoteza 2-1 mbele ya Nkana ya Zambia katika Ligi ya Mabingwa Afrika, leo wanarejea kwenye Ligi Kuu Bara kucheza na KMC kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba inaikabili KMC ambayo iko katika morali kubwa baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Prisons mwishoni mwa wiki.

Wekundu wa Msimbazi wenye pointi 27 wanatakiwa kushinda mchezo huo ili kupunguza presha ya pengo la pointi na Yanga wanaoongoza ligi kwa pointi 44 na Azam iliyo nafasi ya pili kwa pointi 40 lakini zote zikiwa zimecheza michezo 16 tofauti na Simba iliyocheza michezo 12.

Kasi ya Yanga inaonekana kuwapa presha Simba ambao wanataka kutetea ubingwa wao msimu huu na leo kocha wa kikosi hicho Patrick Aussems alisema lazima wahakikishe wanapata ushindi ili kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.

Aussems hajaonyesha kuuhofia mchezo wa leo licha ya kusikia ushindi walioupata KMC dhidi ya Prisons, badala yake ametamba kuibuka na pointi tatu.

Aussems alisema ataingiza kikosi chake uwanjani akitambua wazi kwamba utakuwa mchezo mgumu, lakini lazima wapambane kwa namna yoyote ile ili kupata matokeo na wabakie nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu.

“Tunajua kwamba walishinda kwenye mchezo wao wa mwisho lakini nina ripoti kamili kuhusu hiyo timu, hakika nitapata matokeo kwa sababu nina wachezaji wengi na ninawaamini,” alisema.

Alisema: “Mchezo dhidi ya KMC nitawatumia wale ambao hawakucheza kabisa katika mchezo uliopita. Nitabadilisha kikosi na sina shaka na hao nitakaowapa nafasi kwani ninawaamini na hiyo ndio nafasi ya kuonyesha ubora wao katika mchezo huo,” alisema

Naye kocha wa KMC, Ettiene Ndayiragije, alisema amekiandaa kikosi chake vizuri na kilichobaki ni kucheza tu mchezo huo na kuhakikisha anatoka na pointi tatu.

“Matokeo waliyoyapata Simba dhidi ya Nkana ni matokeo ya mpira kwa hiyo siyaangalii sana na hata kocha wao kama akichezesha wachezaji wengine hainifanyi nikawadharau kwani najua ni usajili ambao aliufanya kwa kuuamini na wachezaji wa Simba wote wapo vizuri, kikubwa mimi naingia nikijua naenda kucheza na Simba,” alisema Ndayiragije.

Wakati huo hio Simba imetangaza viingilio vya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Red Devil’s huku kiingilio cha chini kikiwa sh 3000.

Simba itaikabili Nkana ya Zambia katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili.

Wekundu wa Msimbazi wanatakiwa kushinda bao 1-0 ili kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.



Chanzo: mwananchi.co.tz