Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji Simba mwendo wa dozi tu

89977 Simba+pic Mbelgiji Simba mwendo wa dozi tu

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha Sven Vandenbroeck ameanza kwa neema kibarua chake baada ya kuvuna mabao 10 katika mechi mbili alizoongoza kikosi cha Simba.

Sven alikuwa kwenye benchi kwa mara ya kwanza katika mechi ya Kombe la FA ambayo Simba ilishinda mabao 6-0 dhidi ya AFC Arusha.

Kocha huyo jana aliiongoza Simba kupata tena ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza Lipuli kufungwa idadi kubwa ya mabao katika ligi hiyo tangu ilipoanza Agosti 24, mwaka huu.

Lipuli imefungwa mara mbili kati ya mechi tano ilizocheza dhidi ya Simba tangu ilipopanda Ligi Kuu.

Mshambuliaji nguli Paul Nonga alisema hawakucheza vizuri na makosa waliyofanya yamewagharimu.

Nonga mwenye mabao saba katika ligi, alisema wamefungwa mabao mepesi yaliyotokana na uzembe.

“Tumefungwa mabao mepesi, tumefanya makosa na Simba wakatumia kutuadhibu, tuliingia na malengo ya kushinda lakini hali imekuwa tofauti Simba ilikuwa bora zaidi yetu,”alisema Nonga.

Uzembe wa mabeki wa Lipuli ambao muda mrefu walicheza kwa kujilinda ulichangia timu hiyo kuadhibiwa kwa idadi kubwa ya mabao.

Mfungaji wa mabao mawili Hassan Dilunga alisema dhamira yao ni kupata ushindi katika kila mchezo, hivyo waliingia uwanjani wakiwa na malengo ya kupata pointi tatu.

Simba jana ilimaliza kipindi cha kwanza ikiongoza kwa bao 1-0 huku ikitawala sehemu kubwa ya mchezo huo.

Dakika ya sita beki Gadiel Michael alitengeneza shambulizi zuri, lakini mpira wake wa krosi aliopiga kwa Meddie Kagere uliokolewa na kipa wa Lipuli Agathony Mkwando.

Lipuli ilijibu shambulizi dakika ya tisa kwa kiki kali ya Kenneth Masumbuko akiwa nje ya eneo la hatari iliyopanguliwa na kipa Beno Kakolanya.

Simba ilipata bao la kwanza dakika ya 11 likifungwa na Francis Kahata aliyepokea krosi ya beki Shomari Kapombe aliyepandisha mashambulizi .

Dakika ya 49 Kagere alifunga bao la pili akimfunga kirahisi Mkwando aliyedhani ameotea baada ya mfungaji kupata pasi ya Clatous Chama.

Dilunga atajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi ikiwemo ile ya dakika ya 52 baada ya Simba kufanya shambulizi la kushtukiza lakini alipokwa mpira alipotaka kumpiga chenga beki wa mwisho wa Lipuli.

Dakika ya 56 Simba ilipata bao la tatu likifungwa na Dilunga baada ya mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro kuamuru ipigwe penalti baada ya Novatus Lufunga kushika mpira wakati Chama akitaka kufunga dakika ya 55.

Dakika ya 62 Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwa viungo wawili Jonas Mkude nafasi yake kujazwa na Mzamiru Yassin. Deo Kanda aliingia badala ya Kahata.

Mabadiliko yaliisaidia Simba kupata bao la nne lililofungwa na Dilunga akipokea pasi ya Sharaf Shiboub.

Katika mechi nyingine, Polisi Tanzania licha ya kumkosa kinara wake wa mabao, Ditram Nchimbi aliyesajiliwa na Yanga, ilitumia vizuri uwanja wa nyumbani wa Ushirika Moshi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC.

Polisi Tanzania ilipata bao la kwanza kupitia kwa Marcel Kaheza dakika ya 21 akifunga kwa penalti kabla ya Erick Msagati kupiga la ushindi dakika ya 78. KMC ilipata bao kwa penalti likifungwa na Abdul Hillary dakika 81.

Mabao ya Polisi Tanzania yameivusha kutoka nafasi ya 12 hadi ya sita iliyokuwa imeshikwa na Namungo. Namungo imeshuka hadi nafasi ya saba kwa tofauti ya mabao.

Polisi Tanzania imefunga mabao 13 na imefungwa 12. Namungo ina mabao 11 na imefungwa 11.

Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya tano inalingana pointi na mabao na Polisi Tanzania.

Chanzo: mwananchi.co.tz