Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbappe kwenye utawala wa Vini Madrid

Vinicius Mbappe Mbappe kwenye utawala wa Vini Madrid

Wed, 5 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kylian Mbappe juzi Jumatatu alitimiza ndoto yake ya miaka mingi ya kujiunga na Real Madrid ya Hispania baada ya danadana za muda mrefu.

Mbappe mmoja kati ya wachezaji mahiri duniani amejiunga na kikosi hicho cha kihistoria cha Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akitokea PSG ya Ufaransa ambayo ndiyo timu iliyompa jina kubwa duniani.

Madrid ilimtangaza mshambuliaji huyo ambaye anakwenda kuumiliki Uwanja wa Santiago Bernabeu sehemu ambayo wamepita mastaa wakubwa akiwemo Mfaransa mwenzake Zinedine Zidane, Wabrazili Roberto Carlos, Ronaldo de Lima, David Beckham, Iker Casillas na wengine wengi.

“Sasa napenda kuwaeleza kuwa nimetimiza hitaji la moyo wangu la muda mrefu.

“Napenda kuwashukuru sana mashabiki wa PSG, nilishawahi kusema kuwa nitazungumza nanyi wakati sahihi utakapofika, hivyo nawaeleza kuwa naondoka PSG.

“Nawashukuru kwa kunikuza na kunifanya kuwa mchezaji mahiri duniani, nitaendelea kuwaheshimu na kila siku nitaamini kuwa PSG palikuwa mahali kwangu salama,” alisema Mbappe mwenye miaka 25.

Kabla ya kutangazwa, juzi Jumapili alifanya sherehe iliyohudhuriwa na watu 250 ikiwa ni maalumu kwa ajili ya kuwaaga rafiki zake nchini Ufaransa, lakini pia alikutana na rais wa Ufaransa Emanuel Macron.

Huu umekuwa usajili wa kwanza kabisa mkubwa barani Ulaya, lakini ukiwa pia wa kwanza kwa timu hiyo siku chache baada ya kutwaa ubingwa wa 15 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuichapa Borussia Dortmund 2-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Wembley.

Baada ya usajili huu ambao Mbappe amejiunga na timu hiyo kama mchezaji huru, mashabiki wameonekana kuamini kuwa Madrid ya msimu ujao inaweza kuwa kali zaidi na kuendelea kutawala soka la nchi hiyo pamoja na duniani kwa ujumla.

Mkataba wa miaka mitano, unaonekana kuwa unaweza kumsaidia mshindi huyo wa Kombe la Dunia kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza kwenye historia ya maisha yake ya soka.

Mbappe akiwa na Madrid ataungana kwenye kikosi na mastaa wa timu hiyo Vinicius Jnr na Jude Bellingham, Mbrazili Rodrygo pamoja na kinda mpya wa timu hiyo Endrick, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuwika na timu hiyo msimu huu.

Staa huyo atatakiwa kuhakikisha anaonyesha kiwango cha juu zaidi ili kuonekana kuwa bora zaidi kwenye timu hiyo kwa kuwa Vinicius Jnr ameshaweka jina lake juu na ndiye anatajwa kama bora zaidi kwenye timu hiyo kwa sasa.

Mbrazil huyo amefanikiwa kufunga mabao 24 na pasi 11 za mabao, akiwa tayari ana Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo Mbappe hana, lakini amemzidi kwenye idadi ya mabao ya kufunga kwa msimu.

Mkwaja wake sasa:

Mkataba huu utakuwa wa thamani ya Euro 15 milioni kwa mwaka baada ya kodi na atachukua euro 85 milioni kama bonasi kutoka Real Madrid kwa kipindi cha mkataba wake hii ikiwa ni pamoja na bonasi za makombe atakayotwaa, mabao atakayofunga na dakika atakazocheza.

Jezi namba:

Madrid bado hawajasema atavaa jezi namba gani, lakini kwa kuwa akiwa na PSG alikuwa akivaana namba saba, basi atatamani kuvaa hiyo hiyo kwenye kikosi cha Wahispania hao.

Kama atapewa namba hiyo atakuwa amefuata nyayo za Cristiano Ronaldo, lakini unaweza kuwa mtihani mkubwa kwa kuwa sasa jezi hiyo inavaliwa na staa wa Madrid na mchezaji anayesubiriwa kutangazwa kama mchezaji bora wa dunia mwaka huu, Vinicius.

Hata hivyo, ikikosekana hii, anaweza kuvaa jezi namba 9 ambayo amekuwa mara kwa mara akisema anatamani siku moja kuivaa pia ikiwa inawaniwa na kinda mpya wa timu hiyo Endrick.

Lini ataanza kuichezea Real:

Mbappe kuanzia sasa anasubiriwa kuonekana kwenye michuano ya Euro 2024 na timu yake ya taifa ya Ufaransa, akiwa anakwenda kutafuta ubingwa huo kwa mara ya kwanza kwenye historia ya maisha yake.

Mechi yake ya kwanza akiwa na Madrid inatarajiwa kuwa dhidi ya AC Milan kwenye maandalizi ya msimu mpya, mechi ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Soldier Field, Chicago Julai 31.

Madrid itatamani kumuona Mpappe akiwemo kwenye mchezo huu maalumu kwa ajili ya kutangaza zaidi biashara za klabu hiyo nchini Marekani.

Mechi ya kwanza ya La Liga bado hajaifahamika, lakini mechi ya kwanza kabisa ya mashindano kwa Mbappe itakuwa ile ya UEFA Super Cup ambapo Madrid itavaana na mabingwa wa Kombe la Europa Atalanta, kwenye Uwanja wa Warsaw, Poland Agosti 14.

Akiwa na PSG Mbappe, ambaye alijiunga na timu hiyo akitokea Monaco amekuwa mahiri kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa, baada ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye timu hiyo kwa miaka saba kuanzia mwaka 2017.

Kwa miaka saba misimu sita staa huyo amefanikiwa kufunga mabao 30 na zaidi kwenye mashindano yote.

Msimu Mechi Mabao

2017/18 44 21

2018/19 43 39

2019/20 37 30

2020/21 47 42

2021/22 46 49

2022/23 43 41

2023/24 48 44

308 266

Chanzo: Mwanaspoti