Umeisikia hii? Kylian Mbappe ameripotiwa kukataa kwenda kujiunga na Liverpool kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana baada ya Paris Saint-Germain kumpatia nafasi ya kuachana na miamba hiyo ya Ufaransa.
Lakini, baadaye, Mbappe alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu ya kuendelea kubaki Parc des Princes hiyo mwaka jana baada ya kuhusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Real Madrid.
Ripoti mpya zinadai kwamba Mbappe kwa sasa anataka kuachana na PSG ndani ya mwaka huu baada ya maisha yake kuchukua sura mpya kwenye kikosi hicho cha Paris, Oktoba mwaka jana.
Mkataba wa Mbappe ulivuja mtandaoni wakati mabingwa hao wa Ligue 1 wakifichua kupata hasara ya Pauni 317 milioni.
Jambo hilo limedaiwa kuibua matatizo makubwa kwa mshambuliaji huyo huku akiingia kwenye mgogoro mwingine na fowadi mwenzake, Neymar.
Kocha wa PSG, Christophe Galtier aliitisha kikao cha kikosi chake cha kwanza na wachezaji hao kusuruhishwa, lakini uhusiano wa wakali hao umeshindwa kuwa sawa na kinachoelezwa Mbappe haoni kama ataweza kucheza hadi mwisho wa mkataba wake.
Na tangu hapo, Mbappe ameshindwa kujifunga maisha yake kwenye kikosi cha PSG. Staa huyo alisema: "Kwa sasa, zishapita fainali mbili za Kombe la Dunia. Baada ya hapo, sifahamu itakuwaje." Hiyo ilikuwa kauli ya Mbappe mwaka jana, ambayo iliibua maswali mengi kuliko majibu.
Mbappe alikasirishwa na kucheleweshwa kwa mishahara yake ya hivi karibuni huko PSG jambo linalozidi kubainisha hali isiyofaa baina ya mchezaji na klabu. Kwa mujibu wa The Athletic, PSG iliripotiwa kumruhusu Mbappe aondoke mwaka jana, lakini kwa wakati huo mahali pekee angeenda ni Liverpool.
Ripoti hiyo ilifichua kwamba rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi na mshauri wa klabu, Antero Henrique walihitaji mkwanja wa Pauni 352 milioni kwenye ada ya kumuuza mchezaji huyo, ili kurudisha kiwango cha pesa walizolipa Barcelona mwaka 2017, Pauni 200 milioni kumsajili Neymar.
Hata hivyo, Mbappe hakuwa tayari kwenda Anfield – jambo linaloweka wazi kwamba hana mpango wa kwenda kujiunga na Liverpool na mipango yake ya baadaye ni kwenda Real Madrid.
Na kilichoelezwa ni kwamba hata uamuzi wake wa kubaki Paris na kukataa kwenda Madrid ulikuwa wa kisiasa ulioshinikizwa na Ufaransa na Qatar katika kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2022.
Liverpool waliamua kumsajili straika Darwin Nunez kwa pesa na imewaongoza Luis Diaz na Cody Gakpo kwenye kikosi chao.
Wakati Liverpool wakisajili wachezaji wa kutosha, maisha ya Mbappe huko PSG bado yapo kwenye mashaka makubwa na ikitokea timu anayopenda kwenye ikimtaka, bila ya shaka atamwaga wino kwenda kukipiga kabla ya dili lake kufika tamati Parc des Princes.
Wanaolipwa kibosi PSG
Kylian Mbappe - Pauni 827,000 kwa wiki
Neymar - Pauni 810,000 kwa wiki
Lionel Messi - Pauni 670,000 kwa wiki
Marquinhos - Pauni 238,000 kwa wiki
Marco Verratti - Pauni 238,000 kwa wiki
Sergio Ramos - Pauni 225,000 kwa wiki
Gianluigi Donnarumma - Pauni 215,000 kwa wiki
Keylor Navas - Pauni 198,000 kwa wiki
Achraf Hakimi - Pauni 172,000 kwa wiki
Presnel Kimpembe - Pauni 165,000 kwa wiki
Juan Bernat - Pauni 139,000 kwa wiki