Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbappe kaijibu Arsenal ishu ya kutua Emirates

Mbappe Asema Hendi Real Madrid Mbappe kaijibu Arsenal ishu ya kutua Emirates

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta aliwahi kusema hivi "kila mtu anataka kuichezea Arsenal."

Hayo yalikuwa maneno ya Mhispaniola huyo wakati alipozungumzia uwezekano wa kunasa huduma ya mshambuliaji Kylian Mbappe kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Lakini, kwa wakati huo, Mbappe hakupatikana kuzungumza kwa upande wake ishu ya kwenda Arsenal.

Na hatimaye, amepatikana. Je, amesemaje kuhusu kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Emirates.

Kwa kifupi tu, supastaa huyo, amezima ndoto za siku moja atakwenda kuchezea Arsenal.

Kilichopo na kinachoelezwa ni Mbappe atakapoachana na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu, basi kituo kitakachofuata ni kutimkia zake Real Madrid kwa uhamisho wa bure kabisa kwa kuwa mkataba wake huko Parc des Princes utakuwa umefika tamati.

Kinachoelezwa, Mbappe, 25, amekubali kupunguza hata mshahara wake ili kufanikisha ndoto zake za kwenda kukipiga Los Blancos.

Katika sakata hilo la uhamisho wa Mbappe, miamba ya Emirates, Arsenal nayo ilitajwa kuwa kwenye mchakato wa kuhitaji saini yake na watafanya kweli kumsajili Mfaransa huyo endapo dili lake la kwenda Real Madrid litakuwa halijatiki huku ikidaiwa pia anavutika kupita njia ya shujaa wake mwingine ambaye ni Mfaransa mwenzake, Thierry Henry.

Kitu cha bahati, mkali huyo alikutana na shabiki mmoja wa Arsenal, ambaye alitumia fursa hiyo kumuuliza kama atakuwa tayari kwenda kuvaa uzi mwekundu na mweupe wa wakali hao wa London.

Shabiki huyo alimwambia Mbappe "njoo Arsenal".

Kitu cha kushangaza, Mbappe alianza kucheka na kisha kujibu "hilo haliwezekani".

Mbappe, akaulizwa kwa nini hawezi kwenda London Kaskazini, mkali huyo alijibu: "Kuna baridi sana."

Jambo hilo limewaacha mashabiki wa Arsenal kwenye majonzi makubwa na mmoja alisema: "Ndoto zimeyeyuka."

Shabiki mwingine aliongeza: "Kamwe hakuna hiyo nafasi."

Mashabiki wengine waliendelea kuwa na matumaini atatua Emirates: "Kile kicheko ni cha maana anatupenda, atakuja."

Kocha Arteta alipoulizwa mwezi uliopita kuhusu timu yake kama inavutia mastaa wa maana kwenda kujiunga na miamba hiyo, alisema: "Ndio, kwa nini isivutie? Kama tunataka kuwa timu bora, basi tunahitaji kusajili vipaji bora."

Chanzo: Mwanaspoti