Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbappe hakanyagi nyasi za Santiago Bernabeu kifua mbele

Mbappe X Bernabeu Mbappe hakanyagi nyasi za Santiago Bernabeu kifua mbele

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Inatajwa Dennis Bergkamp alipokuwa usajili wa kwanza wa Kocha Bruce Rioch kila kitu kilibadilika Arsenal. Superstaa alikuwa amefika klabuni. Umri ulikuwa sahihi. Jina lilikuwa kubwa. Ulikuwa mwanzo mpya wa Arsenal mpya.

Wachezaji wengi wakubwa wakatamani kucheza Arsenal. Kucheza kando ya fundi Dennis. Alitokea Inter Milan. Kabla ya Inter Milan alikuwa Ajax. Mchezaji mkubwa aliamsha ari klabuni. Baadaye akaja Arsene Wenger. Kilichoafuata ni historia.

Maili kadhaa kutoka London, kuna jiji linaitwa Manchester. Kuna timu inaitwa Manchester United. Supastaa, Eric Cantona alitua klabuni hapo akitokea Leeds United ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1992.

Cantona alipotua United kila kitu kikabadilika. Akawa mchezaji mkubwa zaidi aliyetua katika mikono ya Sir Alex Ferguson. Akabadili mawazo ya wachezaji na mashabiki. Akawaongoza katika nchi ya ahadi. Baadaye hata wachezaji wakubwa wakatamani kucheza Manchester United.

Majuzi usiku maandiko yakatimia pale Santiago Bernabeu. Baada ya hisia za muda mrefu, hatimaye mapenzi yakafanyika juu ya kitanda. Kylian Mbappe alitangazwa rasmi kuwa mchezaji wa Real Madrid. Ilishaanza kutuchosha kuhusu uvumi wa Mbappe na Real Madrid.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni utambulisho. Wenzetu utambulisho ni biashara. Mashabiki wananunua tiketi kwa wingi kwenda kushuhudia mchezaji akiingia uwanjani kwa mara ya kwanza na jezi mpya ya klabu yao. Anapigana danadana na kuongea maneno machache. Klabu inaingiza mabilioni.

Wakati Mbappe atakapokuwa anaingia uwanjani Santiago Bernabeu kutambulishwa, kichwa chake kitakuwa chini. Sawa, ndoto imetimia. Lakini ana deni kubwa moyoni. Anaingia Madrid kama mchezaji wa kawaida tu. Jina kubwa lakini mchezaji wa kawaida.

Ana bahati mbaya hawezi kwenda Real Madrid halafu ujio wake ukawa kama ule wa Bergkamp Arsenal au Cantona pale Manchester United. Anakwenda kuamsha nini ambacho hakijawahi kufanywa?

Siku nne kabla hajatambulishwa kuwa mchezaji wa Real Madrid, wenzake walikuwa London wakitwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Upande wa kushoto, Vinicius Junior kama kawaida yake alikuwa akiiteketeza Borussia Dortmund.

Hii inaashiria Mbappe haingii Madrid kama staa ambaye anaenda kuiamsha timu. Hapana. Msimu huu ulioisha tayari wenzake wameshashinda kila kitu. Mbappe anakuja kujibu baadhi ya maswali machache tu mgumu.

Swali la kwanza. Ataweza kuepuka mkosi maarufu kama gundu ambao amekuwa nao PSG? Pale Paris Mbappe alicheza kando ya mastaa wengi wakubwa wakiwemo Lionel Messi na Neymar lakini hakuweza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Msimu wake wa kwanza tu kama Madrid wakitolewa katika hatua yoyote ya michuano hiyo watu watasema Mbappe amepeleka gundu.

Hata kama Real Madrid wakifika fainali kisha wakapoteza mechi bado wataamini ni mkosi ambao umepelekwa klabuni na Mbappe. Madrid hawajawahi kupoteza pambano la fainali tangu mwaka 1983 wakati walipopoteza kwa Aberdeen ya Scotland ambayo ilikuwa inafundishwa na Sir Alex Ferguson.

Lakini kuna swali jingine ambalo tunasubiri kutoka kwa Mbappe. Atakwenda kucheza nafasi gani pale Santiago Bernabeu. Mbappe anakuwa bora akitokea upande wa kushoto. Anahitaji kukimbia katika nafasi kubwa upande wa pembeni, huku akiingia katika boksi la adui na kupiga chenga huku akifunga.

Ni upande huo huo ndio ambao Vinicius amekuwa akifanya kazi zake vyema. Sijui ni nani atahamia upande wa katikati au kulia. Kocha Don Caro atajua namna ya kufanya lakini sisi ni watazamaji wa kawaida tu kama wakati ule Luis Figo na David Beckham walivyocheza pamoja miaka ya nyuma.

Tajiri kama Florentino Perez kazi yake kubwa ni kukusanya wachezaji bora waliopo sokoni. Hata kama wanacheza nafasi moja. Ni jukumu la kocha kujua nani atakwenda kucheza wapi.

Hawezi kumwacha Mbappe sokoni, tena akiwa anapatikana bure eti kwa sababu anacheza upande mmoja na Vinicius. Hapana.

Swali jingine ambalo ni gumu kwa Mbappe ni kama ana uwezo wa kuwa mwanasoka bora wa dunia kabla ya Vinicius Junior. Tunajua ambacho kimempeleka Real Madrid. Anajua atakuwa katika nafasi nzuri ya kuwa mwanasoka bora wa dunia. Ufaransa ina uwezo wa kumpa nafasi hiyo lakini PSG walikuwa hawana uwezo wa kumpa nafasi hiyo.

Sasa hivi atakuwa ana uwezo wa kuchukua nafasi hiyo akiwa na Real Madrid pamoja na kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kama ambavyo Zinedine Zidane amewahi kufanya huko nyuma. Hata hivyo Mbappe anaweza kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia kabla ya Vinicius Junior?

Anaweza kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia kabla ya Jude Bellingham? Wabrazil wakitwaa Kombe la Mataifa ya Amerika Kusini, au Waingereza wakitwaa Euro basi Vinicius na Jude watakuwa katika nafasi nzuri ya kuwa wanasoka bora wa dunia kwa sababu kwanza tayari wana taji la Ligi ya mabingwa wa Ulaya. Ni hata kama Mbappe atatwaa Euro na Wafaransa, wenzake tayari wana taji la Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Lakini kuanzia hapo hapo alipo, Mbappe amejipeleka katika timu ambayo wapinzani wenzake wa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia wapo hapo hapo. Jude na Vinicius. Litakuwa jambo la kushangaza kidogo lakini ilishawahi kutokea hapo zamani.

Vyovyote ilivyo, Mbappe haendi Madrid kifua mbele. Hadi baada ya msimu ujao tutajua kama atakuwa mfalme wa Madrid au hapana. Kwa sasa tayari kuna Wafalme pale Real Madrid.

Ana kazi ngumu na kuutoa ufalme katika mikono ya waliopo na kisha utue katika mikono yake.

Chanzo: Mwanaspoti