Kylian Mbappe ameandika rekodi mpya wakati chama lake la Ufaransa likiendeleza ubabe wake wa asilimia 100 kwenye mchakamchaka wa kufuzu michuano ya Euro 2024 baada ya kuichapa Ugiriki 1-0 mjini Paris.
Mkwaju wa penalti uliopigwa dakika 55 na Mbappe ulimfanya afunge bao lake la 54 ndani ya mwaka huu na hivyo kumpiku Just Fontaine kwa kuwa Mfaransa aliyefunga mara nyingi kwa klabu na timu yake ya taifa ndani ya mwaka mmoja.
Hata hivyo, mkwaju wake wa kwanza ulipanguliwa na kipa wa Ugiriki, Odysseas Vlachodimos kabla ya mwamuzi kuamuru penalti irudiwe.
Kolo Muani na Jules Kounde nao walikuwa na nafasi nzuri ya kufunga, kabla ya Ugiriki kuwa na wakati mgumu baada ya Konstantinos Mavropanos kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Muani katika dakika 69 ya mchezo.
Kwenye mechi nyingine ya Kundi B, Ireland iliwachukua dakika 52 kuvunja ngome ya beki ya Gibraltar kabla ya kufunga mabao yao kupitia kwa Mikey Johnston, Evan Ferguson na Adam Idah na hivyo kuondoka uwanjani kwa ushindi wa 3-0 katika mchezo uliofanyika mjini Dublin.
Kwenye Kundi C, Ukraine walijiona wenye bahati baada ya kujihakikishia nafasi ya pili nyuma ya England, iliyoichapa North Macedonia 7-0. Ukraine ilishinda 1-0 dhidi ya Malta huko Trnava, shukrani kwa bao la mkwaju wa penalti la Viktor Tsygankov.
Kundi D, Armenia nao ilikuwa na bahati kwa kupata penalti ya dakika za majeruhi na kushinda 2-1 dhidi ya Latvia, huku Wales wakichapwa 2-0 na Uturuki, wakati kwenye Kundi H kulikuwa na hat-trick ya Daniel Hakans, aliyesaidia Finland kupata ushindi wa kibabe wa mabao 6-0 dhidi ya San Marino.
Slovenia na Denmark ilifungana 1-1 huko Ljubljana, jambo linalowafanya Kazakhstan kupanda hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Northern Ireland huko Belfast. Kundi I, Uswisi na Romania iliisha 2-2.