Mchezaji wa Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) Kylian Mbappe, ametangaza rasmi kuondoka katika klabu hiyo baada ya kuhumudu ndani ya klabu hiyo kwa miaka saba.
Mbappe ambaye ni mshindi wa Kombe la dunia Mwaka 2018 ametangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo amesema ni mwaka wake wa mwisho PSG na hataongeza mkataba kwenye klabu hiyo.
Mbappe amesema mechi yake ya kesho Jumapili Mei 12, 2024 dhidi ya Toulouse ndio itakuwa mechi yake ya mwisho akiwa mchezaji wa PSG.
Mbappe ambaye alijiunga na PSG kwa Mkopo Mwaka 2017 akitokea Monaco ya Ufaransa, leo amewaaga Mashabiki wa Klabu hiyo huku akibainisha kuwa anaenda kuanza maisha mapya nje ya Ufaransa.
Katika mazungumzo yake amewaahidi Mashabiki wa Klabu hiyo kuwa ataendelea kuiunga Mkono klabu yake pedwa ya PSG hata akiwa nje ya Ufaransa ambapo atakuwa anatazama michezo mabalimbali ya klabu hiyo kupitia runinga.
Mchezo wake wa Mwisho akiwa na Jezi ya Matajiri hao wa Jiji la Paris atacheza jumapili ya May 12 dhidi ya Toulouse saa nne usiku kwa saa za Afrika mashariki.
Ni zaidi ya Misimu miwili sasa Mbappe amekuwa akihusishwa kujiunga na Real Madrid lakini kila ifikapo dirisha la usajili juhudi za Madrid kumsajili Huwa zinagonga mwamba.
Licha ya Kugonga mwamba kwa kipindi kirefu lakini bado taarifa kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa tayari Mbappe ameshasaini mkataba na mabingwa hao wa muda wote wa UEFA Champions League, Real Madrid ambapo atakwenda kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu.
Mbappe akiwa na PSG,amecheza michezo 306, amefunga mabao 255,pasi za mabao 108, ameshinda mataji yote ya ligi 1 na PSG, Kombe la Ufaransa mara tatu, Kombe la Ligi mara mbili na Super Cup ya Ufaransa mara nne.
Unatamani kumwona Mbappe anasaini timu gani?