Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint- Germain Kylian Mbappe amesifiwa na mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kiwango bora anachoendelea kuonyesha.
Mbappe alikuwa shujaa katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Lyon kwani alicheka na nyavu mara mbili kwenye mechi ya Ligue 1 mwishoni mwa juma lililopita.
Mbappe alifunga bao la mapema kupitia mkwaju wa Penati baada ya mchezaji wa Lyon, Corentin Tolisso kumchezea rafu Manuel Ugarte, kabla ya Achraf Hakimi hajapachika bao la pili bao la nne likiwekwa na Marco Asensio.
Katika mchezo huo Lyon iliweka rekodi ya kufungwa mabao manne dhidi ya PSG kipindi cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996.
Sasa Mfaransa huyo amefunga mabao matano katika mechi tatu alizocheza baada ya kurejea dimbani kufuatia mvutano wake na mabosi wa PSG kuhusu mkataba.
Mbappe alitemwa kikosini baada ya kugoma kusaini mkataba mpya na kuwekwa sokoni katika dirisha la usajili la kiangazi.
Aidha juma lililopita taarifa ziliripoti Mbappe anapanga kutatua ishu yake na mabosi wa klabu hiyo baada ya mvutano wa muda mrefu kuhusu mkataba.
Kwa mujibu wa ripoti Mbappe atasaini mkataba mpya na PSG utakaodumu hadi mwaka 2026, katika mkataba huo utajumuisha kipengele kipya utakaomwezesha kusajiliwa na Real Madrid.