Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbappe alivyoiweka dunia katika mfuko wake

Mbappe Record Kylian Mbappe

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mwingine dunia unaweza kuiweka mfukoni. Unaishi katika dunia ambayo unaitawala. Dunia ambayo unatingisha na inakunyenyekea. Dunia ambayo unaibabaisha. Nimecheka namna ambavyo Kylian Mbappe amefanya ndani ya miezi 12 iliyopita.

Mwaka jana alisaini mkataba mpaka wa miaka mitatu na PSG. Mkataba wa miaka miwili ulikuwa lazima halafu mwaka mmoja ungeweza kuwa chaguo. Mbappe aliacha kilio kule Hispania kiasi kwamba La Liga walilazimika kuandika taarifa ndefu ya kuishutumu PSG kwa kile walichodai kwamba huenda klabu hiyo ilikuwa imekiuka kanuni za matumizi ya pesa kwa mujibu wa UEFA.

Ilichekesha. La Liga iliwahusu nini? Rafiki anakubaliana kuendelea kuishi na mkewe lakini kumbe inakuumiza. Inakuhusu nini? Ndicho ambacho kiliwatokea La Liga. Baada ya kuwapotezs Cristiano Ronaldo na Lionel Messi walitamanj kupata majina makubwa ambayo yangeibeba Ligi Kuu ya Hispania.

Wakati huo, Erling Haaland alikuwa ametangazwa kwenda Manchester City. Mbappe alikuwa ametangaza kubakia Ufaransa japo awali mwelekeo ulikuwa unaonekana kwamba angeenda Real Madrid iliyokuwa imeafikiana naye maslahi binafsi. Lakini ghafla pesa za Waarabu wa PSG zikambakisha.

Inadaiwa mwenyewe alipewa kiasi cha Euro 100 milioni ili asaini mkataba mpya kwa sababu tayari alishakuwa mchezaji huru. Lakini PSG walikubali kumlipa mshahara wa Euro 500,000 kwa wiki. Kufikia hapo Mbappe mwenyewe alinyoosha mikono, ingawa tamaa yake ilikuwa kucheza Real Madrid.

Nani hataki kuichezea Real Madrid? Timu kubwa zaidi ya kihistoria Ulaya. Timu ambayo Zinedine Zidane, Robert Carlos, Ronaldo de Lima, David Beckham, Raul Gonzalez na mastaa kibao duniani wamecheza. Timu ambayo inaongoza kwa kutwaa mataji mengi ya Ulaya. Nani hataki kucheza katika timu kama hii.

Hata hivyo, noti za Waarabu zilikuwa na ushawishi mkubwa kwa Mbappe. Siku hizi Real Madrid na ndugu zao Barcelona hawana ubavu wa kupambana na pesa za Waarabu. Kama linakuja suala la pesa hawana ubavu huo. Labda kwa wale wachezaji wachache ambao wanathamini ukubwa wao na historia zao katika soka ndio wanaamua kwenda huko.

Lakini ghafla Mbappe amebadilisha mawazo yake kwa sasa. Anadai kwamba msimu ujao utakuwa wa mwisho kwake kucheza PSG ingawa angeweza kutanua mkataba wake mpaka mwisho wa msimu. Mashabiki wa timu yake wamechukia. Kila mtu Ufaransa amechukia.

Kwanini amebadilisha mawazo yake? Sio ngumu sana kujua. Kwanini amebadilisha mawazo. Inawezekana wakati mwingine pesa sio kila kitu. Unahitaji vitu vingine kando ya pesa. Kwa mfano, kwa mara nyingine tena Mbappe amekwama kutwaa taji la ubingwa wa Ulaya akiwa na PSG. Messi ameondoka na Neymar anaondoka.

Kuna kila dalili kwamba mradi uliotengenezwa na PSG kuchukua ubingwa wa Ulaya unaonekana kukwama na labda Mbappe hawezi kusubiri tena. Hali ni tete. Unapokwenda katika timu kama Real Madrid unajiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Na unapochukua ubingwa wa Ulaya unajiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Ubingwa wa Ufaransa pekee haukuhakikishii nafasi ta kuchukua tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Labda Mbappe ameanza kugundua ukweli huu na kuhisi kuna timu nyingine kubwa inaweza kumpa nafasi hiyo.

Mfano ni namna ambavyo Kelvin De Bruyne na Haaland walivyojiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia mwishoni mwa msimu. Wapo mbele ya Mbappe kwa sasa. Kama hawatakuwepo hata katika tatu bora watu watashangaa sana. Katika Ligi ngumu kama ya England, Haaland na De Bruyne wametwaa mataji matatu ikiwemo Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Achilia mbali jambo hilo kuna ukweli kwamba kuna timu ambazo zina mvuto mkubwa wa kihistoria. Mfano ni Real Madrid. Kuna wachezaji wachache duniani ambao waliwahi kukataa kuvaa jezi nyeupe za kihistoria za Real Madrid. Hata Mbappe alipoamua kusaini mkataba mpya na PSG huku akiwa mchezaji huru tulimshangaa kidogo.

Hata hivyo niliwahi kuandika humu kwamba Mbappe alikuwa ananunua muda tu kwa sababu mpaka saaa umri upo katika upande wake. Hakuwa na haraka. Wakati anaikataa Real Madrid alikuwa na miaka 23. Ilikuwa rahisi kwake kuvuta muda kwa sababu angeweza kwenda Madrid akiwa na miaka 25 au 26 na bado asingekuwa amechelewa.

Hata huyu Haaland ambaye tunamuona kwa sasa ukweli ni kwamba ananunua muda tu. Ana miaka 22 na anaweza kujikita Manchester City kwa sasa huku akinunua muda tu. Katika umri wa miaka 26 anaweza kuamua kwenda zake Real Madrid au Barcelona na asiwe amechelewa. Wachezaji wanaopaswa kuwahi kwenda huko ni akina Harry Kane sio yeye.

Pamoja na yote haya ni wakati mwafaka pia kwa Mbappe kwenda kujipima katika Ligi iliyo bora zaidi ya ile ya Ufaransa. Hii Ligi ya Ufaransa huwa inaitwa Ligi ya wakulima. Haichukuliwi kwa umakini mkubwa kama zilivyo ligi za England na Hispania. Wapo wanaoamini pia kuwa Ligi za Italia na Ujerumani ni bora kuliko Ufaransa.

Wenzake wengi ambao anacheza nao Ufaransa walishajipima katika Ligi nyingine. Mfano ni kama akina Messi, Neymar, Ashraf Hakimi na wengineo walishajipima kwingineko na baadae wakaamua kwenda Ufaransa kuchota pesa. Ni wakati mwafaka kwa Mbappe kwenda kujipima kwingine.

Muda anao, pesa anazo, kipaji anacho na huu ni wakati wake kusumbua. Hakuna Ronaldo wala Messi. Dunia inamtazama zaidi yeye. Ameiweka katika kiganja. Anaifanya analotaka. Ni kama ambavyo mwaka jana tu aliamua kusaini mkataba wa kubakia PSG lakini ghafla mwaka huu ameamua kubadilisha mawazo yake.

Chanzo: Mwanaspoti