Wakati ishu ya Kylian Mbappe ikiwa moto kutaka kuuzwa, imeelezwa kuwa kama Paris Saint-Germain wasipotimiza masharti, basi staa huyo atasaini mkataba wa awali na Real Madrid.
Mbappe alitangaza kuwa, hataongeza mkataba wa kuendelea kuichezea Paris Saint-Germain pindi akimaliza mkataba wa sasa mwaka 2024.
Taarifa zinaeleza kuwa, Paris Saint-Germain inaweza kulazimika kumuuza staa wake huyo endapo tu ataendelea kukomaa kutoongeza mkataba.
Mara ya mwisho wakati Mbappe anasaini mkataba wake wa sasa, alikubaliana na Paris Saint-Germain kuwa katika mkataba huo atapatiwa kiasi cha euro 150m.
Inaelezwa kuwa, Mbappe ataondoka ndani ya Paris Saint-Germain kama timu hiyo itashindwa kumlipa kiasi cha euro 150m, fedha ambayo walimuahidi wakati anasaini mkataba wake wa sasa.
Ripoti zinaeleza kuwa, kama Paris Saint-Germain wasipompa kiasi hicho cha fedha, basi Mbappe atasaini mkataba wa awali na Real Madrid ikifika Januari Mosi mwakani.
Wakati hayo yakiendelea, Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, inaelezwa anahitaji huduma ya nyota huyo ndani ya kikosi hicho ili kuziba nafasi ya Karim Benzema aliyetimkia Al-Ittihad ya Saudi Arabia.