Baada ya kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote ndani ya Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe amefunguka kuwa, anaangalia namna gani atafunga na kuifanya timu hiyo ifuzu mbele ya Bayern Munich.
Bayern Munich na Paris Saint-Germain wanatarajiwa kuvaana leo Jumatano pale Allianz Arena, Munich, Ujerumani, ukiwa ni mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mchezo wa awali Paris Saint-Germain wakiwa nyumbani, walipoteza kwa bao 0-1 dhidi ya Bayern Munich.
Staa huyo wikiendi iliyopita alifikisha mabao 201, akivunja rekodi ya Edinson Cavani ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote klabuni hapo akiwa na mabao 200.
Mbappe amesema kwa sasa anaangalia kuwa ni namna gani ataifungia timu yake mabao ili wafuzu kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Kwanza najivunia kuichezea Paris Saint-Germain, ni kitu spesho kwangu kuwa mchezaji wa timu hii, nipo katika jiji langu la Paris kuandika historia, nataka kuwa na mafanikio nikiwa hapa.
“Kwa sasa nahifadhi mabao yangu kwa ajili ya mechi ya Bayern Munich, nitaendelea kupambana kuona nashinda na timu yetu inafuzu.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunajiamini na kwenda kupambana na Bayern kuona tunashinda,” alisema Mbappe.