Timu ya Mbao imeshindwa kutakata katika uwanja wake wa nyumbani CCM Kirumba baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na maafande wa Rhino Rangers ya Tabora.
Mtanange huo wa First League umepigwa leo uwanja wao wa nyumbani ukiwa ni mchezo wa pili kwa wabishi hao wa Kanda ya Ziwa, mechi ya kwanza wakiibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Nyaishozi ya Kagera.
Licha ya timu zote kucheza kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa za mabao lakini timu hizo zililazimika kwenda mapumziko milango ikiwa bado migumu kwa pande zote, huku kipindi cha pili kila timu ikicheza kwa tahadhari kuhakikisha walau inaondoka na alama moja, ambapo hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika Mbao 0-0 Rhino Rangers.
Matokeo hayo yanaifanya Mbao kufikisha pointi Saba katika mechi nne walizocheza wakisogea hadi nafasi ya pili nyuma ya Mbuni yenye alama Saba, huku Rhino wakifikisha alama tano katika nafasi ya nne kwenye kundi B lenye timu nane.
Kocha wa Mbao, Godfrey Chapa amekiri kuwa safu ya ushambuliji ya timu yake inamuangusha kwa kutokufika eneo husika kwa wakati na kuzitumia vyema nafasi zinazotengenezea huku akiwataka wachezaji kuipambania thamani ya nembo ya timu hiyo na kuhakikisha wanafanya vizuri dhidi ya Alliance.