Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbao, Alliance zashuka daraja 

Mbao Pic Data Mbao, Alliance zashuka daraja 

Tue, 20 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mkosi wa kushuka daraja umeendelea kuziandama Mbao FC na Alliance FC ambazo sasa zimeporomoka kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na kuangukia Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya kufanya vibaya katika mechi walizocheza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Vipigo ambavyo timu hizo imevipata kutoka kwa Fountain Gate Academy na Kitayosce Jumamosi na Jumapili vimezifanya zisiwe na uwezo wa kumaliza juu zaidi ya nafasi nne za mwisho kwenye msimamo wa kundi B la Ligi Daraja la Kwanza hivyo kushuka rasmi kimahesabu.

Kwa mujibu wa kanuni za FDL msimu huu, timu nne zitakazoshika mkia katika kila kundi zitashuka daraja hadi Ligi Daraja la Pili

Alliance ambao walifungwa mabao 3-1 nyumbani na Fountain Gate Academy jana Jumapili, wamebaki na pointi tano na hata wakishinda mechi zao tatu zilizosalia dhidi ya Mbao, Rhino Rangers na AFC, watafikisha jumla ya pointi 14 ambazo hazitoweza kufikia pointi za Transit Camp walio katika nafasi ya tano ambayo ni ya kucheza mchujo wa kuwania kubaki.

Kwa Mbao wenyewe ni kama ilivyo kwa Alliance kwani kwa pointi saba walizonazo, hata wakishinda mechi tatu walizobakiza dhidi ya Alliance, AFC na Transit Camp bado watamaliza katika nafasi nne za chini kwenye kundi hilo na hivyo itashuka daraja.

Kocha wa Mbao FC, Ammy Ninje amesema kilichowaangusha katika mashindano hayo ni uzoefu mdogo wa wachezaji wao.

"Kuna vitu vidogovidogo kwa sababu hawa hawana uzoefu hivyo vinawatoa mchezoni. Mimi kama mwalimu nitaendelea tu kuwajengea hali ya kujiamini na tujaribu kumalizia mechi zilizobaki," alisema Ninje.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz