Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazoezi ya Ten Hag kama huna moyo utakimbia timu - Staa afunguka

Rahford Mataja Ten Hag.jpeg Ten Hag na Rashford

Sun, 5 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Erik ten Hag amerudisha soka la mvuto Manchester United — lakini unaambiwa hivi, mazoezi ya kocha huyo ni magumu kwelikweli na kuwapa wakati mgumu wachezaji katika siku za mwanzo, ikiwamo mazoezi ya wachezaji 11 dhidi ya 0.

Hilo linafichuliwa na staa wake wa zamani huko Go Ahead Eagles, ambayo ilikuwa timu yake ya kwanza Ten Hag kwenye ukocha.

Sjoerd Overgoor alikuwa sehemu ya kikosi cha Go Ahead Eagles ambapo mastaa wake walipata shida kubwa kuelewa njia za ufundishaji za Ten Hag wakati alipowasili kwenye klabu hiyo ya Uholanzi majira ya kiangazi mwaka 2012.

Overgoor alisema: “Wachezaji wengi walikuwa wakidhani, ‘huyu kocha kichaa’. Baada ya mechi ya pre-season, alitufanyisha mazoezi ya wachezaji 11 dhidi ya sifuri. Alitupanga kila mchezaji kwenye nafasi yake, kuanzia kwa kipa, anaanzisha mpira kwa beki wa kati wa upande wa kushoto na baada ya hapo tunaendelea. Ilikuwa inaboa kwa sababu hakukuwa na timu pinzani. Tulifanya hivyo mara nyingi sana na wachezaji walikuwa wakisema, ‘Tena? 11 dhidi ya sifuri?’.”

Hiyo ina maana Ten Hag aliwapanga wachezaji 11 kucheza wenyewe tu wakiwa timu moja bila ya mpinzani uwanjani. Na Overgoor alisema kama ilivyowakuta mastaa wa Man United, Cristiano Ronaldo kabla hajaondoka na Marcus Rashford — kukumbana na adhabu kali kutoka kwa kocha huyo, hiyo ndiyo staili yake ya kuwafanya wachezaji wawe na nidhamu tangu yupo Eagles.

Overgoor, 34, alisema Ten Hag hapendi wachezaji wavivu kwenye kikosi chake na anataka kila mchezaji ahusike kwa asilimia 10 na zaidi na kama kutakuwa na mchezaji mwenye kujitolea kwa asilimi 80 au 90 na anaridhika, basi atampigia kelele muda wote. Kuhusu nidhamu Overgoor alisema: "Ten Hag kama utachelewa mazoezini, hufanyi mazoezi. Alikuwa na sheria zake kutufanya kuwa profesheno.”

Ten Hag alipoondoka Eagles alitimkia Bayern Munich kuinoa timu B kabla ya kwenda kufanya makubwa Ajax na sasa anarudisha zama bora huko Man United, ambapo katika miezi yake michache kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, tayari ameshashinda ubingwa wa Kombe la Ligi na bado kikosi chake kipo kwenye mchuano wa kuwania ubingwa wa mataji matatu yaliyobaki, Ligi Kuu England, Kombe la FA na Europa League.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live