Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele balaa zito 2022, mkali wa dabi

Mayele Fiston Kalala Fiston Mayele

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hapana shaka mwaka 2022 utakuwa wa kihistoria kwa nyota wa Yanga, Fiston Mayele kutokana na ubabe aliouonyesha katika kufumania nyavu kulinganisha na mastraika wengine wa timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Licha ya kutoibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliomalizika ambao ulianzia mwaka 2021 na kumalizikia 2022, Mayele ndani ya mwaka huu ameonyesha muendelezo mzuri wa kufumania nyavu kulinganisha na wenzake, jambo ambalo hapana shaka linamuweka katika daraja la tofauti.

Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti, imebaini kuwa Mayele ndiye mchezaji aliyekuwa tishio zaidi katika kufumania nyavu ndani ya mwaka 2022 na hilo linajidhihirisha kwa takwimu zake ambazo ameziweka akiwa anakitumikia kikosi cha Yanga.

MTEMI LIGI KUU

Kwa sasa, Mayele ndiyo kinara wa kufumania nyavu katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu ambapo hadi sasa amefumania nyavu mara 14 lakini takwimu zinaonyesha ndiye mchezaji aliyepachika idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi Kuu ndani ya mwaka huu ambapo amefunga mabao 25.

Msimu uliopita, kiujumla, Mayele alipachika mabao 16 lakini kati ya hayo, mabao matano tu ndiyo alifunga mwaka 2021 na mabao 11, aliyafunga mwaka huu hivyo ukiyajumlisha hayo na 14 aliyofunga hadi sasa unapata idadi ya mabao 25 kwa mwaka 2022.

Katika msimu uliopita, mabao 11 ambayo Mayele aliyafunga mwaka huu aliyapata katika mechi dhidi ya Coastal Union aliyoifunga matatu, Kagera Sugar (2) na Mbeya Kwanza, Mtibwa Sugar, Geita Gold, Biashara United, Namungo na Azam ambazo kila moja aliifunga bao mojamoja.

Mabao 14, aliyopachika msimu huu ni dhidi ya timu za Singida Big Stars aliyoifunga mabao matatu kama alivyofanya dhidi ya Coastal Union, Dodoma Jiji (2), Mbeya City (20 na Polisi Tanzania (2) wakati timu za Azam na Mtibwa Sugar amezifunga bao mojamoja.

ACHANUA KIMATAIFA

Ukali wa Mayele katika kufumania nyavu ndani ya mwaka huu haujajidhihirisha katika ligi ya ndani tu bali pia katika mashindano ya klabu Afrika.

Ndani ya mwaka huu, Mayele ameichezea Yanga katika mechi sita za mashindano ya kimataifa ambazo ameifungia timu yake jumla ya mabao saba.

KINARA HAT TRICK

Fiston Mayele ndiye mchezaji aliyeongoza kufunga idadi ya mabao matatu kwa mchezo mmoja (hat trick) kulinganisha na wengine wanaozitumikia timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara katika mashindano tofauti katika mwaka huu.

Mayele amefunga hat trick mara tatu ambapo mbili ni dhidi ya Zalan FC katika Ligi ya Mabingwa Afrika na moja dhidi ya Singida Big Stars.

TISHIO UGENINI

Fiston Mayele ameonyesha uwezo wa kufunga katika viwanja tofauti kwenye Ligi Kuu jambo ambalo siyo rahisi kwa wachezaji wengi hasa wale wa kigeni.

Katika mabao 25, ambayo Mayele ameyafunga kwenye Ligi Kuu mwaka huu, nyota huyo kutoka DR Congo, amefumania nyavu mara 10 akiwa akiitumikia Yanga katika mechi za ugenini huku mabao 15 akiifungia pindi wakiwa katika uwanja wa nyumbani.

MKALI WA DABI

Ndani ya mwaka 2022, Fiston Mayele ndiye mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao katika mechi zinazokutanisha timu zinazotoka katika eneo moja (dabi)

Katika mwaka huu, Mayele amefunga jumla ya mabao manne katika mechi tano za dabi ambapo mabao mawili amefunga dhidi ya Simba kwenye Ngao ya Jamii na mawili amefumania dhidi ya Azam FC katika Ligi Kuu.

Chanzo: Mwanaspoti