Mshambuliaji wa zamani wa Reli na Kagera Sugar, Seleman Msagasumu amesema aina ya uchezaji anaocheza straika wa Yanga, Fiston Mayele anahitaji kiungo mpiga pasi za mwisho ili aendelee kufunga zaidi.
Kutokana na hali hiyo, Msagasumu ameishauri Yanga iliyoachana na Saido Ntibazonkiza isajili mchezaji mwingine mwenye uwezo wa kupiga pasi za mwisho zaidi ya watu iliyonayo kwa sasa.
Msagasumu, aliyewahi kuichezea CDA alisema Mayele analijua lango, lakini ni lazima awe na usadizi wa kutengenezewa nafasi.
Alisema Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni mchezaji mzuri, ila anahitaji usaidizi wa mtu mwingine mwenye uwezo wa kupiga pasi za mwisho.
“Kuna pasi inasema straika nenda pale kimbilia pale hizi huwa zinapigwa na viungo mafundi niliona katika mchezo wa Simba dhidi ya KMC, Kibu Denis alimpigia Pape Ousmane Sakho na kufunga sasa Yanga inahitaji mtu wa namna ile, ili Mayele azidi kutetema,” alisema.
Msagasumu pia alishauri timu hiyo kutafuta beki wa kushoto mpya mwenye uwezo wa kupiga krosi ili kuendelea kutengeneza mabao kupitia pembeni.
“Soka limebadilika mnaweza mkabanwa katikati ya ywanja, ila ni lazima mtumie flangs sasa mabeki wa kulia na kushoto na lazima wawe watu wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi,” alisema.
Juu ya ushiriki wa michuano ya CAF, Msagasumu alisema atafutwe mtu mwenye kimo kirefu wa kucheza na Bakar Mwamnyeto eneo la beki wa kati.
Alisema mashindano ya Kimataifa timu huwa zinatumia udhaifu mdogo kuweza kupata matokeo.
“Dickson Job, bonge la beki lakini kimo chake anaokabana nao watakuwa wanapiga mipira ya juu tu,mimi namkubali sana lakini ni lazima waangalie hili linaweza kuwa ni tatizo,” alisema.