Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele anavyoipaisha Yanga

Mayele Caf.jpeg Fiston Mayele

Wed, 24 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara na kikosi cha Yanga, Fiston Mayele amezidi kuwa moto mkali katika kufumania nyavu za wapinzani wake na kuiweka timu yake kwenye rekodi tamu.

Bao pekee la juzi alilofunga Uwanja wa Liti dhidi ya Singida Big Stars Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) lilitosha kuifanya Yanga kutinga fainali na kwenda kutetea ubingwa huo itakapokutana na Azam Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwenye Shirikisho Afrika mabao mawili aliyofunga Uwanja wa Mkapa Aprili 23 mwaka huu dhidi ya Rivers katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya robo fainali yalitosha kuivusha Yanga hatua ya nusu fainali sababu mchezo wa pili zilitoka suluhu.

Katika mchezo wa mwisho hatua ya nusu fainali dhidi ya Gallants ambapo Yanga ilishinda ugenini mabao 2-1, Mayele alifunga bao moja kama ilivyo kwa Kennedy Musonda na kufanya mshambuliaji huyo kufikisha mabao sita sawa na Ranga Chivaviro wa Gallants.

Mayele ndio kinara wa mabao msimu huu wakati ligi ikiwa imesalia michezo miwili akiwa na mabao 16 na kuweka tumaini kubwa la kunyakua kiatu cha ufungaji bora.

Mwishoni mwa wiki hii Yanga itakutana na USM Alger kwenye mchezo wa kwanza wa fainali Uwanja wa Mkapa na tayari ikiwa imeshatetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Kinara wa mabao wa ASFC hadi sasa anaongoza, Andrew Simchimba mchezaji wa Ihefu mwenye mabao saba akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao sita huku mfungaji bora wa msimu uliopita alikua, Abdul Seleman 'Sopu' kwa mabao yake tisa akiwa Coastal Union.

Sopu ndiye mchezaji aliyemfunga mabao mengi kipa wa Yanga, Djigui Diara tangu atua Jangwani amefungwa mabao matano, matatu kwenye fainali ya ASFC msimu uliopita na mawili kwenye ligi na sasa wanakutana tena.

Mayele tangu ajiunge na Yanga msimu uliopita alipofunga mabao 15 na sasa 16 hajawahi kufunga bao la penalti licha ya kupewa nafasi hiyo amekuwa akikosa penalti zake.

Msimu uliopita alikosa penalti katika suluhu dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Mkapa na msimu huu alikosa katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Hii ni fainali ya pili, Yanga kukutana na Azam kwani mara ya kwanza zilikutana msimu wa mwaka 2015/16 na Yanga kushinda maba 3-1 na unaonekana utakuwa mchezo wa kisasi kwa kila mmoja.

Azam inasaka kombe lake la pili kwani 2018/19 ilitwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa Lipuli bao 1-0 lililofungwa na Obray Chirwa Uwanja wa Ilulu, Lindi huku Yanga ikisaka kombe lake la saba.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Wille Martin 'Gari Kubwa' alisema;

"Mapinduzi ya soka haya ndio watu walikuwa wanayalilia miaka yote na hii inalifanya soka letu kuwa na thamani kubwa kwa kufanya kwao vizuri."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: