Mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara zinaonekana zimeegemea kwa Fiston Mayele peke yake huku akitamba kutaka kuivunja rekodi yake mwenyewe ya mabao 16 na ya George Mpole aliyemaliza mfungaji bora kwa mabao 17 msimu uliopita.
Msimu huu Mayele ameifikia rekodi yake ya msimu uliopita kwa kufunga mabao 16 na amebakiza mechi mbili dhidi ya Mbeya City na Prisons kuivuka na kutengeneza mpya huku anayemfuata ni Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.
Kwenye mabao ya msimu huu kuna baadhi ya timu amezifunga nje na ndani huku nyingine akizifunga mara moja na baadhi ya timu hajazifunga kabisa.
Coastal Union imefungwa na Mayele mabao matatu msimu huu kama ilivyo kwa Singida Big Stars wakati Polisi Tanzania na Mbeya City zikifungwa mabao mawili huku Mtibwa, Kagera Sugar, Ihefu na Azam zikifungwa bao moja moja.
Timu za Ruvu Shooting, Simba, KMC, Geita Gold na Namungo hajizaguswa kabisa na Mayele msimu huu lakini baadhi ya timu hizo msimu uliopita zilionja makali ya straika huyo.
Timu pekee ambazo zimembania Mayele kutikisa nyavu zao msimu huu na uliopita kwenye Ligi Kuu ni Simba, Ruvu Shooting na Prisons ambayo bado ina mechi dhidi ya Yanga itakayofanyika Mei 28.
Kama Prisons itambania mchezaji huyo asifunge basi itakamilisha idadi ya timu tatu ambazo zimekuwa ngumu kwa Mayele kuzifunga kwa misimu miwili mfululizo ikiwemo Simba ambayo ameshamalizana nayo pamoja na Ruvu Shooting.
Kwa ujumla timu ambayo imeonewa sana na Mayele ndani ya misimu yake miwili akiwa ndani ya jezi ya Yanga ni Coastal Union ambayo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita ikifuatiwa na Mtibwa Sugar iliyofungwa mabao manne huku Azam, Dodoma Jiji na Singida zikichapwa mabao matatu na straika huyo raia wa Congo .
Mayele alisema kwa sasa anataka kuhakikisha anaisaidia Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na akirejea atazipangia mkakati mechi mbili za ligi zilizobaki kuhakikisha anavunja rekodi yake na kuweka mpya.
"Bado nina hamu ya kuchukua ufungaji bora baada ya msimu uliopita kuukosa. Najua mechi zimebaki mbili lakini ngoja tuzingatie kwanza mechi ya kimataifa iliyo mbele yetu halafu sasa nikirudi nitazipangia mkakati hizo mechi mbili zilizobaki kuhakikisha nafunga.
"Nashukuru nimefikia rekodi yangu ya mabao ya msimu uliopita na sasa nataka kuhakikisha mechi hizo mbili naivunja rekodi hiyo na kuweka mpya, msimu wa ligi ulikuwa mgumu lakini niseme hakuna beki aliyenipa wakati mgumu uwanjani ila jambo ambalo nililiona ni timu nyingi kukamia mechi hasa zinapokuja kucheza na sisi.
"Hizi timu za majeshi ni kazi sana kucheza nazo kwa sababu wanatumia nguvu kubwa sana sasa lazima kuwa makini nao na ucheze nao kwa akili, najua nina mechi dhidi ya Prisons ambayo sijawahi kuifunga lakini acha kwanza tusubiri kuona itakuaje," alisema Mayele.