Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele "ampasua" kichwa Kocha wa USM Algiers

Mayele Hdfsgs.jpeg Fiston Mayele

Wed, 31 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Licha ya USM Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 wakiwa ugenini kwenye mchezo wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga, kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha anaumiza kichwa namna ya kumdhibiti Fiston Kalala Mayele ambaye anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali.

Juni 3, Yanga itakuwa ugenini, Stade du 5 Juillet, Algiers kuvuja jasho kwa mara nyingine tena ili kupindua matokeo kwenye fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambalo huu ni msimu wa 20 tangu kuanzishwa kwake 2004.

Akizungumza na Mwanaspoti, Benchikha alisema bado wana kazi kubwa na ngumu ya kufanya wakiwa nyumbani kwenye mchezo wa marudiano kutokana na ubora wa Yanga ambao wamekuwa wakiuonyesha kwenye michezo ya ugenini.

"Zitakuwa dakika 90 nyingine ngumu hasa kutokana na aina ya matokeo ambayo yamepatikana kwenye mchezo wa kwanza, tunatakiwa kuwa makini licha ya kwamba tutakuwa nyumbani huku tukiwa na faida ya mashabiki wetu.

"Tulijiandaa kukabiliana na Yanga huku tukijua ubora wao ulipo, tulijitahidi kuwa na nidhamu kubwa kwenye kujilinda lakini tukajikuta tukiruhusu bao, yule mshambuliaji wao (Mayele) ni hatari hivyo tunatakiwa kuwa na mpango mwingine wa kukabiliana naye kwenye mchezo wa marudiano.

"Ni mshambuliaji asiyetabirika mwenye nguvu, kasi na maarifa hivyo anaweza kuwa na madhara wakati wowote. Kiukweli hakuna kocha asiyetamani kuwa naye.

"Tulimfuatilia kwa muda mrefu na tuliamini kuwa hawezi kupata bao lolote, lakini katushtua na kufunga bao zuri, nafikiri tunakwenda tukiwa tunafahamu kuwa tunatakiwa kuwa makini naye, tutajiandaa vizuri kwa ajili ya hilo.

"Hatuwezi kusema kazi imemalizika kwa sababu kwenye soka lolote linaweza kutokea tunatakiwa kuona ni kama tumepoteza hivyo tunatakiwa kufanya kila ambalo linawezekana ili kufanya vizuri tena kwenye fainali ya pili," alisema.

Bao ambalo alifunga Mayele kwenye mchezo huo wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ni la saba na limemfanya kumzidi kete Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants ambaye awali alikuwa naye sawa kwa mabao sita sita.

Kwa sasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa DR Congo ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hiyo ambayo Yanga imeingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kutinga hatua ya fainali kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake miaka 19, iliyopita.

Licha ya Yanga kupoteza kwenye fainali ya kwanza ikiwa nyumbani, inarekodi ya kufanya vizuri ugenini, ilifanya hivyo dhidi ya Club Africain (1-0) kwenye hatua ya mchujo, ikaifunga TP Mazembe (1-0) kwenye hatua ya makundi, pia Rivers United (2-0) na Marumo Gallants (2-1) kwenye hatua ya robo na nusu fainali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live