Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele ajifunze kwa Chama

Mayele X Chama  Mayele ajifunze kwa Chama

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Fiston Kalala Mayele ni mchezaji ambaye amekuwa akipendwa zaidi Yanga kwa miaka hii miwili kuliko mchezaji mwingine yeyote.

Mabao yake na bila ya shaka, staili yake ya kushangilia kwa “kutetema” ni vitu ambavyo vitabaki katika historia na mioyo ya Wanayanga milele.

Haina ubishi kwamba Yanga ikiwa na Mayele imeshinda mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, mawili ya ASFC na Ngao ya Jamii mara mbili, zote ikiifunga Simba kwa mabao ya Mayele.

Na Mayele pia alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita iliyoenda pia kwa Saido Ntibazonkiza wa Simba kila mmoja alipofunga mabao 17, huku pia akiandika historia mpya katika maisha yake kwa kushinda tuzo ya Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita kwa mabao yake saba.

Na kubwa katika yote Mayele aliiwezesha Yanga kuandika historia mpya kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1935.

Kuondoka kwa Mayele kuliwastua Wanayanga, ambao walishazoea kutetema katika staili ambayo ilionekana kuwavutia hata wapinzani, ambao wengine licha kukiri ilikuwa ikiwapasua moyo, lakini wakiwa peke yao walivutika kutetema kimtindo wajaribu angalau kuonja ladha yake wajue ukitetema unakuwa katika hali gani.

Kiufupi ilikuwa ni staili iliyotingisha soka la Tanzania na maisha kiujumla. Bungeni, kwenye nyumba za ibada, kwenye bendi za dansi, kwenye Bongo Muvi na komedi, shuleni na maeneo mbalimbali; watoto vijana kwa wazee tena wa jinsi zote mbili walitetema. Ni staili iliyokamata kikwelikweli na kuchangia Mayele kupendwa mno na hata wasio mashabiki wa mpira.

Lakini katika siku mbili zilizopita, staa huyo raia wa DR Congo ameliamsha baada ya kuonyesha shaka yake kwamba huenda alifanya makosa kuja kucheza soka Tanzania.

Katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Chuki ya nini mimi sio Mtanzania bhona nilikosea kucheza timu za Tanzania ni nini.”

Mmoja akamjibu: “@mayelefiston hao watakuwa mashabiki wa Simba achana nao kaka.”

Mayele naye akajibu: “…. Sio mashabiki wa Simba ni mashabiki wa Yanga nawajua vizuri.”

Na Haji Manara wa Yanga akaandika: “My brother Pls futa hii sio nzuri.”

Shabiki mwingine akaandika: “Mayele sisi mashabiki wa Tanzania hususani Yanga tunakupenda ila kuna baadhi wachache waliumia kutokana na kuondoka kwako. Mimi mwenyewe ni shabiki wa Yanga nilikuwa sifuatilii Ligi ya Misri lakini toka umejiunga nao nimekuwa mfuatiliaji mkubwa. Hilo ni la kwanza, la pili ukiwa na timu ya Congo mechi zenu za saa tano usiku nafuatilia, nalala saa saba ili nikuone kipenzi chetu ila nilikuwa naumia sana kocha alipokuwa anakunyima nafasi, una uwezo mkubwa sana…. Hivi unamuona Harry Maguire Man United hapendwi ila hasikilizi kelele za mashabiki na ukizifuatilia sana utapotea, we fanya kazi yako.”

Hizi ni kati ya meseji chache zilizoandikwa chini ya mnyororo ulioanzishwa na Mayele na zinaonyesha jinsi ambavyo wapo watu wengi sana ambao wanaendelea kumpenda straika huyo wa mabao.

Hofu yake kwamba alikosea kuja nchini sio sahihi.

Kwa sababu Mayele hakuwa akijulikana Afrika kabla hajaja Yanga. Hakuwahi kuwa mfungaji bora wa Afrika kabla hajaja Yanga na pia hakuwahi kucheza fainali ya Afrika kabla hajaja Yanga.

Na pia alikuwa hajawahi kuchezea timu ya taifa ya DR Congo kabla hajaja Yanga. Na hata kocha wa timu ya taifa ya DR Congo, Sebastien Desabre hakumwita katika kikosi cha timu ya taifa kilichoenda kwenye fainali za Mataifa ya Afrika kule Ivory Coast, kwa kuvutiwa na pozi anazoweka pale kwenye benchi la timu ya Pyramids kule Misri, bali ni kwa sababu ya moto aliouwasha alipokuwa Yanga.

Ndio Yanga ilikuwa haijawahi kufika fainali ya Afrika kabla ya Mayele, lakini Mayele pia alikuwa hajawahi kucheza fainali ya Afrika kabla hajatua Yanga. Hii ni “win win situation.”

Hivyo Mayele hapaswi kuona alikosea kuja kuchezea timu ya Tanzania, kwa sababu ndio imemfanya awe huyu Mayele anayetajika Afrika na imempa dili la kutua huko Misri.

Kwa namna yoyote, Mayele anapaswa kuishukuru Yanga na sio kukerwa na mashabiki wachache wa mitandaoni au viongozi wachache anaodai waliwahi kumwambia kuwa “hatafunga mabao na lazima atarudi Yanga.” Hao viongozi wachache waliomkera ama kumkebehi ama “kumfanyia hila za giza” kama anavyohofia, watapita na Yanga itabaki palepale. Na heshima aliyoijenga Yanga itabaki kama jinsi jina alilolipata Yanga litakavyoendelea kumpa maokoto huko aendako.

Utata huu uliozuka, umewafanya mashabiki kuanza kumkumbusha Mayele kwamba yeye si wa kwanza kuwa mfungaji bora Afrika kwani mzawa Mrisho Ngassa alishawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika pale alipofunga mabao sita msimu wa 2014 na kwamba hajawahi hata kumfikia mzawa mwingine Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ anayeshikilia rekodi ya Ligi Kuu Bara kwa kuifungia timu hiyo ya Wananchi mabao 26 katika ligi mwaka 1997.

Maneno ya mashabiki hayawezi kwisha.

Hana sababu ya kujibizana na watu na wala hana sababu ya kuhofia “kutupiwa majini”, kama uvumi na utani unaoendelea kutrendi huko kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kutofunga mabao kwa Mayele pale Pyramids na timu yake ya taifa ya DR Congo, ambayo imemaliza katika nafasi ya nne kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023.

Mchezaji aliyeondoka vibaya Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alifanya mgomo wa miezi kadhaa kabla ya kuombewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aachiwe aende, yuko zake Azam FC na amekuwa mtamu pengine zaidi ya alivyokuwa Yanga, akifunga mabao manane kufikia sasa, rekodi ambayo hakuwahi kuifikia akiwa Jangwani. Mbona huyu hajafanyiwa hila asifunge?

Wachezaji ambao wamekuwa wakizipa nafasi imani za ushirikina, daima wameishia kwenye aibu na Mayele hapaswi kuingia huko. Akimweka Mungu mbele hakuna kitakachomzuia kwa sababu ni yeye, Mungu, anayempa mtu mafanikio na wakati mwingine kumnyang’anya mafanikio hayo ili aone utamshukuru ama utamkufuru.

Lakini kwa magumu anayopitia Mayele, sio mbaya akajifunza jambo kwa Clatous Chotta Chama na Luis Miquissone wa Simba. Waliondoka Simba wakiwa katika kiwango cha juu kabisa wakitamba Afrika, wakaenda kujiunga na timu za Uarabuni, RS Berkane na Al Ahly, mtawalia. Walipofika huko walishindwa kung’aa. Wakaondoka. Hawakusema walikosea kuchezea timu za Tanzania. Walipotakiwa tena na Simba walirudi kwa amani na mambo yanawaendea vyema.

Tanzania ni nchi ya upendo sana, Mayele. Hukukosea kuja kucheza hapa.

Chanzo: Mwanaspoti