Mshambuliaji kinara wa Klabu ya Yanga, Fiston Kalala Mayele amesema kuwa wao kama wachezaji wamepokea kwa mikono miwili ahadi ya rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa Tsh milioni 5 kwa kila bao watakalofunga katika michuano ya CAF.
Raia huyo wa Congo amesema hayo baada ya kutua Dar es Salaam na kikosi cha timu yake wakitokea Tunisia ambako walicheza na US Monastir na kuambulia kipigo cha bao 2-0 na kusema kuwa malengo yao jkwa sasa ni kusaka alama tatu dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa katika Dimba la Mkapa Jumapili, Februari 19, 2023.
"Mechi itakuwa ngumu kwa sababu TP Mazembe ni timu kubwa na nzuri lakini tunawafahamu, lakini kwa vile tutakuwa nyumbani, tutapambana kuchukua alama tatu. Kukamiwa kwa mchezaji ni kawaida, nimewahi kucheza mechi nyingi nakamiwa lakini nafunga.
"Wananchi hawawezi kukata tamaa mechi ya kwanza kwa sababu tuna mechi nyingi, tatu za nyumbani na mbili za ugenini kwa hiyo tutapambana. Dabi ya Congo tutaileta hapa Tanzania.
"Alichokifanya Rais Samia ni motivation nzuri kwa wachezaji, lakini pia timu wameweka bonus ambayo ni hamasa kubwa kwetu wachezaji. Hii ni mechi ambayo tunataka ushindi, mechi zote za nyumbani tunataka ushindi. Lakini sio ushindi tu, lazima watu wateteme kwa sababu hawajatetema siku nyingi, naishia hapo,” amesema Mayele.