Mshambuliaji wa Klabu ya Yanga Fiston Mayele amesema anasubiri kikao cha mwisho na viongozi wa klabu hiyo kwani ndicho kitakachoamua kama anabaki au anaondoka klabuni hapo.
Akihojiwa na Mpenja TV, Mayele ambaye ni raia wa Congo DR amekuwa akihusishwa kutaka kuondoka klabuni hapo baada ya kufanya vizuri kwa misimu miwili mfululizo na kupata ofa kubwa kutoka Afrika Kusini na Uarabuni.
"Kwa sasa mimi ni mchezaji wa Yanga na kuhusu tetesi za kuondoka ni kawaida kwa sababu nimefanya vizuri ila nasubiri kikao cha mwisho ndio nitajua kama nitaondoka au nitaendelea kubaki.
"Sisi wachezaji wa Kikongo tunapenda hela na hapa nimekuja kutafuta hela ila hata Kama nitaondoka sitaondoka kwa fujo wala makelele.
Licha ya kufanya siri kubwa, lakini TanzaniaWeb inajua kwamba vigogo wa Yanga juzi usiku walikuwa na kikao kizito na Fiston Mayele nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Mayele mwenye mkataba wa mwaka mmoja na Yanga amegoma kusaini mkataba mpya ambao ungemfanya awe analipwa pesa ndefu kuliko mchezaji yeyote ndani ya timu hiyo huku akidaiwa amepagawa na ofa nono kutoka Esperance ya Tunisia, Zamalek, Pyramids za Misri, timu za ubelgiji na Qatar.
Kikao hicho kilihusisha pia wasimamizi wa mchezaji huyo ambao wanapushi staa huyo akiwashe Arabuni ambako kuna mkwanja mnene na wako tayari kununua mkataba uliosalia Yanga
Bado hawajafikia muafaka wa kusalia au kuondoka ingawa tajiri ahidi dau nono lakini juzi mchana alionekana kwenye sehemu Jijini Dar es Salaam akipiga picha za matangazo ya uzi mpya wa Jangwani ambao umetangazwa jana usiku nchini Malawai.
Mshambuliaji huyo kupiga picha na uzi wa Yanga kwa ajili ya tangazo ni jambo ambalo linaashiria lolote linaweza kutokea.