Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Kalala Mayele amesema kuwa licha ya Yanga kupoteza kwa kushindwa kubeba Ngao ya Jamii mbele ya Simba anaamini bado timu hiyo ina uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa ligi kuu kutokana na ubora ambao bado upo katika kikosi hiko.
Mayele kwa sasa ni mchezaji halali wa klabu ya FC Pyramids ya nchini Misri ambao wamemsajili kutoka Yanga baada ya msimu uliopita kumalizika baada ya kufanya vizuri ikiwemo kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika na kuisaidia Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo iliyo chini ya Shirikisho wa Soka Afrika.
Akizungumza nasi, Mayele alisema kuwa, licha ya Yanga kushindwa kubeba taji mbele ya Simba lakini anaamini kuwa hiyo sio sababu ya wao kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi ambapo ameweka wazi kuwa Yanga bado ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kutwaaa ubingwa katika msimu huu.
“Yanga sio kwamba wameshindwa kutwaa ubingwa mbele ya Simba basi wasiwe na vigezo vya kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu, Yanga wanatimu nzuri sana na yenye wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.
“Bado wanayo nafasi kubwa sana ya kutwaa ubingwa wa ligi kwa msimu huu mpya, wanacheza mpira mzuri sana na naamini tayari walishapata muunganiko mzuri ambao naamini utawafanya kupata matokeo mazuri katika michezo yao ijayo,” alisema mchezaji huyo.